MWANDISHI WETU-DODOMA
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuipatia Tanzania mkopo nafuu kujenga barabara ya njia nne kuanzia Morogoro hadi Dodoma ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.
Dk. Mpango ametoa ombi hilo jana jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo anayewakilisha nchi nane za ukanda wa Afrika Mashariki, Amos Cheptoo.
“Barabara hii ilijengwa muda mrefu miaka ya 80, malori mengi yanapita hapa kwenda Mwanza, Kigoma na nje ya nchi, ikiwemo Burundi, Rwanda na unaona kabisa imeelemewa na imeanza kuharibika,” alisema Dk. Mpango.
Alisema amemwomba Mkurugenzi Mtendaji huyo wa AfDB waanze kuliweka jambo hili kwenye miradi itakayogharimiwa na benki hiyo baadaye ili barabara hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuelekeza magari mawili kwenda upande mmoja na mengine mawili kupita upande mwingine iweze kujengwa.
“Baada ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, tunahitaji usafirishaji kwa njia ya barabara uwe na tija zaidi, uende haraka zaidi, lakini pia kupunguza ajali. Hivi sasa kuna ajali nyingi sana kwa sababu magari yanayokwenda Dar es Salaam na yanayokuja Dodoma au kwenda Mwanza yanapishana kwenye haka kanjia kamoja,” alisema Dk. Mpango.
Kwa upande wake, Cheptoo aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, alisema benki yake itahakikisha Tanzania inapata mikopo ya miradi yake ya kimkakati na ya kipaumbele, ukiwemo huo wa barabara ya Morogoro hadi Dodoma.
Katika hatua nyingine, Cheptoo ameitaka sekta binafsi nchini kuchangamkia fursa za mikopo nafuu zilizopo AfDB.
“Sekta binafsi hapa Tanzania haijatumia vizuri dirisha la mikopo ya sekta hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine za ukanda huu wa Afrika na ninakuomba Mheshiiwa Waziri wa Fedha na Mipango uihamasishe sekta binafsi ikope fedha hizo ili kukuza mitaji yao na kuongeza tija,” alisema Cheptoo.
Aidha, alisema kuwa AfDB ipo katika hatua za mwisho za kutoa fedha kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Dodoma.
Alisema tayari benki hiyo imetoa fedha kwa ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma pamoja na miradi mipya ya kuzalisha nishati ya umeme ambayo iko mbioni kuwasilishwa katika vikao vya bodi hivi karibuni.
Cheptoo amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuwa kiongozi mwenye maono, ambaye amesaidia katika mabadiliko makubwa ya uchumi na kuzitaka nchi nyingine barani Afrika kujifunza kutoka Tanzania.
“Nilipotua nimeona jengo la abiria la Terminal III katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, daraja la juu la Mfugale na ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea kwa kasi, miundombinu ambayo miaka miwili iliyopita sikuikuta nilipotembelea hapa nchini,” alisema Cheptoo.
AfDB imefadhili miradi 23 hapa nchini ikiwemo 21 ya umma na miwili ya sekta binafsi, katika nyanja za nishati, miundombinu ya barabara, usafiri, kilimo, maji na usafi wa mazingira, yote kwa pamoja ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 2.1.