22.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Meya Arusha ajiunga CCM

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MEYA wa Jiji la Arusha kwa tiketi ya Chadema, Kalisti Lazaro amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala, Humphrey Polepole katika ofisi ndogo ya Lumumba, Dar es Salaam.

Akizungumza katika kipande kidogo cha video ambayo ilisambazwa na Polepole jana, Lazaro alisema amekuwa akifanya kazi ya umeya katika mazingira magumu.

Alisema ugumu huo amekuwa akiupata pale anapotaka kumsifia kiongozi wa Serikali kwa utendaji kazi, hasa Rais Dk. John Magufuli, lakini amekuwa akipelekewa barua nyingi za kuonywa kwa kumsifia kiongozi huyo wa nchi.

“Nimeshaletewa barua nyingi za kuonywa kwa ajili ya kumsifu Rais. Siwezi kukaa kwenye chama ambacho kimejiondoa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, chama ambacho Kamati Kuu inakutana wanafanya maamuzi makubwa kwa saa mbili.

“Leo Arusha nzima imeenda kuwa CCM, inakuwaje mjumbe wa Kamati Kuu, diwani na meya chama chako hakishiriki? Hii ni sawa na timu imetoka uwanjani na kama imejiondoa maana yake wewe mchezaji unatafuta timu nyingine ambayo inashiriki ligi,” alisema.

Lazaro alisema kwa kuwa CCM inaendelea na uchaguzi na kwa sababu ana nia njema, hivyo atabaki na timu ambayo iko uwanjani.

Mbali na sababu hiyo ya Chadema kujitoa kwenye uchaguzi, Kalisti pia alisema chama hicho kimekuwa na migogoro mingi ya ndani ambayo hawezi kuitaja kwa kuwa yeye sio msemaji wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

“Lakini sio hicho tu, chama chetu kimekuwa na migogoro mingi ya ndani na sitaki kuyasemea maana mimi sio msemaji wao, lakini nichukue nafasi hii kuwaambia wananchi wa wa kata yangu kuwa nitakuja kuwatumikia kwa nafasi ambayo Mungu na chama changu kipya wataamua,” alisema.

Alisema kwa sasa atarudi Arusha kuungana na wenyeviti wa CCM wanaogombea ambao kwa zaidi ya asilimia 99 wameshashinda.

Kwa upande wake, Polepole alisema Lazaro alifika katika ofisi hiyo ndogo CCM Lumumba na kueleza nia yake ya kutaka kujiunga na chama hicho tawala.

“Ndugu Kalisti amesema amepokea barua za maonyo mara kadhaa kutoka uongozi wa Chadema, zikimtaka kutokutoa ushirikiano na viongozi wa Serikali ambao anatakiwa kufanya nao kazi ngazi ya mkoa na wilaya na kutompongeza hadharani Rais Magufuli.

“Vitisho vya mara kwa mara ikiwamo dhidi ya uhai wake ndio vimepelekea kujivua nafasi zake zote katika Chadema na kujiunga na CCM, chama ambacho kinashughulika na utatuzi wa kero za wananchi.

“Pia ameeleza kuwa yuko tayari kuchapa kazi ya wananchi akiwa ndani ya CCM na kwamba yuko tayari kwa maelekezo ya kazi kutoka Uongozi wa CCM,” alisema Polepole.

Aidha alisema Lazaro atapokewa rasmi na wanachama wa CCM Mkoa wa Arusha katika tarehe itakayopangwa hivi karibuni.

Siku za nyuma, Lazaro amekuwa akinyooshewa kidole na makada wenzake wa Chadema kuwa amekuwa akikisaliti chama chake kwa kuisifia Serikali iliyoko madarakani.

Kutokana na hilo, Lazaro mwenyewe mara kadhaa amekuwa akikanusha madai hayo ya kukisaliti chama chake.

MTANZANIA ilipomtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Chadema, Tumaini Makene, ili kuzungumzia Kalisti kujiunga CCM ikiwa bado mwaka mmoja wa kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, alisema kuwa wanamtakia kila la heri.

“Kama ambavyo tuliwaambia wale wote waliokihama chama, tunamtakia kila la heri huko alikokwenda,” alisema Makene.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles