25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TRA sasa mlango kwa mlango

Na Mwandishi wetu, Kisarawe

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka wananchi kujenga utamaduni wa kudai na kuchukua risiti yenye kiwango sahihi kila wanapofanya manunuzi au kupata huduma ambayo wamelipia.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Richard Kayombo, aliyasema hayo juzi wakati wa maadhimisho ya wiki ya huduma, elimu na usajili wa walipakodi, ambapo maofisa wa mamlaka hiyo wanawatembelea wafanyabiashara kwenye maduka yao na kuwapa elimu.

Akiwa wilayani Kisarawe, Kayombo alisema ni kosa kisheria mtu yeyote anapofanya manunuzi ya bidhaa au kupata huduma aliyolipia bila kudai risiti kwa kuwa anaikosesha Serikali mapato.

Kayombo alisema kutokudai risiti kunaweza kumwingiza mtu matatani na kutozwa faini ya kuanzia Sh 30,000 hadi milioni 1.5  au jela kwa muda usiozidi mwaka mmoja au vyote kwa pamoja kutegemea na thamani ya bidhaa au huduma uliyoilipia.

“Ni wajibu wa kila mwananchi kudai na kuchukua risiti kwa kuwa kodi hiyo ndiyo inayotumiwa na Serikali kuleta maendeleo kwa kutekeleza miradi ya barabara, vituo vya afya na huduma zingine za jamii”, amesema Kayombo 

Kayombo aliongeza kuwa TRA inafanya wiki maalumu ya kutoa elimu kwa walipakodi na wananchi kwa ujumla ili kuongeza uelewa wa masuala ya ulipaji kodi na kuwaeleza wananchi faida za kulipa.

“Kampeni hii ni endelevu na tutapita mikoa yote kuwaelimisha walipakodi na wananchi juu ya ulipaji kodi kwa hiari na faida zake kwa wananchi,”alisema.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Mussa Gama, alitoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wa Wilaya hiyo kutumia fursa hiyo kupata elimu na huduma za ulipaji kodi na hatimaye walipe kodi stahiki.

“Nimefurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na TRA ili kuhakikisha kuwa huduma muhimu za ulipaji kod zinawafikia wananchi wa Kisarawe na hivyo natoa wito kwa wananchi wetu watumie fursa hii kupata elimu ya ulipaji kodi kwa kuwa faida inarudi kwa wananchi,”amesema Gama.

Nao wafanyabiashara waliotembelewa katika maduka yao, walipongeza utaratibu wa kufuatwa madukani kwao na kupewa elimu ya kodi na kuitaka TRA kuendelea kuelimisha wafanyabiashara na wananchi ili kila anayestahili kulipakodi alipe kwa hiari.

Ramadhani Idi ambaye ni mkazi wa Kisarawe alisema elimu inayotolewa imempa ujasiri kwa sababu amefahamu kulipa kodi ni lazima na amejifunza mengi na sasa hatawaogopa wala kufunga biashara anapowaona maofisa wa TRA wakienda dukani kwake.

“Kwa kweli nimejifunza mengi na napenda niwaambie wafanyabiashara wenzangu kuwa TRA kwa sasa ni marafiki tusiwaogope wala kufunga biashara pale wanapotutembelea”, amesema

TRA inafanya wiki ya huduma, elimu na usajili wa walipakodi kwa kuwatembelea wafanyabiashara katika maduka yao na kufanya semina za mabadiliko ya sheria za kodi, kodi ya majengo, kodi ya mapato, kodi ya zuio, kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na mambo mengine ya ulipaji kodi ili kujenga uelewa wa masuala ya kodi miongoni mwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla. Kampeni hii ilianza katika mikoa ya Morogoro na Pwani Novemba 11.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles