29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Mtoto huyu ameliza watu

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

HUZUNI na simanzi vilitawala jana kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya Lingston Zambi na Winifrida Lyimo wakati wa kuwasili kwa mtoto, Anna Zambi, ambaye alipoteza wazazi wake wake wote  na wadogo zake watatu kwa ajali ya gari mkoani Tanga.

Wazazi wa binti huyo mwenye umri wa miaka 16, pamoja na wadogo zake watatu Lulu, Andrew na Grace walifariki dunia katika ajali ya gari wakati wakielekea katika mahafali ya kuhitimu kidato cha nne ya binti huyo Oktoba 26 mwaka huu.

Wanafamilia hao walifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakitumia kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.

Baada kutokea ajali hiyo ndugu wa familia hiyo walilazimika kutomweleza mtoto huyo taarifa za kifo cha wazazi wake ili kumwezesha kushiriki vema mitihani yake ya kuhitimu elimu ya sekondari.

Kulingana na taarifa za watu wa karibu wa familia hiyo walilazimika kutomweleza mtoto huyo taarifa hizo hata baada ya kumaliza mitihani yake hadi pale alipowasili jana alfajiri akitokea Handeni Tanga alikokuwa akisoma katika shule ya Sekondari ya Mather Theresia of Calcuta.

Baba mdogo wa mtoto huyo, Ibrahim Zambi alisema kuwa baada ya binti huyo kuwasili nyumbani kwao hapo jana walitumwa watu wanne kumpatia taarifa hizo ambazo zilimfanya aangue kilio na kuamsha majonzi na hali ya simanzi miongoni mwa watu waliokuwa mahali hapo.

Zambi alisema kuwa walilazimika kutomweleza taarifa hizo hata baada ya kuhitimisha mitihani yake kwa sababu walishindwa kufahamu namna ya  kuanza kumpa taarifa hiyo ya huzuni.

“Kwa kweli alilia sana kiasi cha kuwaliza watu waliokuwa hapa nyumbani. Na baada ya kuingia ndani alijilaza miguuni mwa bibi yake na kuendelea kulia kwa muda mrefu,” alisema Zambi.

“Mtoto alilia sana huku akisema alihisi jambo hilo kwa sababu kuna wakati alikuwa anaamka usiku na anadai hata mitihani yake amefanya kwa taabu sana,” alisema Zambi.

Jana mtoto huyo alipelekwa na ndugu zake kwenda kuona makaburi ya wazazi wake na wadogo zake na  maneno aliyokuwa akitamka wakati akilia kwa uchungu ndiyo yaliyowafanya watu wengi waliokuwapo nyumbani hapo na wale waliokuwa wakifuatilia habari zake kupitia mitandao ya kijaamii kulia. 

Akipelekwa kwenda kuangalia makaburi hayo, alionekana akitembea kwa shida huku akiwa ameshikiliwa huku na huku na zaidi alikuwa akilia huku akitamka maneno ya uchungu.

Naona wivu nikiona watoto wenzangu, nasikia huzuni, sisi mama yetu alituzaa bila faida, mama yetu alituzaa kwa uchungu jamani mimi,”. 

“Baba nisamehe mwanao, mimi ndio niliyesababisha mtoto wako kipenzi wa kiume Andrew ameondoka kwa sababu ya upumbavu wangu, ulituzaa ili uje uone matunda yetu” alisema huku akilia kwa uchungu baada ya kufika kuona makaburi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles