GRACE SHITUNDU -DAR ES SALAAM
HATUA ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuelekeza mahakama zote nchini kutoa dhamana kwa mshtakiwa mwenye Kitambulisho cha Taifa au wenye vitambulisho hivyo kuwadhamini watu ambao kesi zao zinadhaminika, inaonyesha kwamba bila kukimiliki, huko mbele ya safari mambo yanaweza kukuwia magumu.
Juzi wakati wa shughuli ya kuwaapisha manaibu wasajili wa mahakama na mahakimu wafawidhi kukabidhiwa vitendea kazi, Jaji Mkuu aliwasisitiza mahakimu kutoa dhamana endapo mshtakiwa atakuwa na kitambulisho cha taifa (uraia) kwani akikimbia atakuwa amejihukumu kwa kukimbia uraia wake.
Kauli hiyo ya Jaji Mkuu imekuja ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu gazeti moja (sio Mtanzania) kuandika kwamba mtu asiye na kitambulisho cha taifa hawezi kupata ajira.
Gazeti hilo lilinukuu tangazo la ajira lililotolewa na sekretarieti ya ajira ambayo iliweka kigezo kimojawapo kwa watu wote wanaoomba ajira serikalini kuhakikisha wanakuwa na kitambulisho cha taifa.
Tangazo hilo lilieleza kwamba kutokana na mabadiliko yaliyofanywa katika mfumo wa ajira nchini, waombaji walitaharifiwa kuwa kuanzia mwishoni mwa Septemba kuwa na vitambulisho vya taifa.
Umuhimu wa kitambulisho cha taifa ulionyeshwa pia na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tangu Mei, mwaka huu baada ya kutangaza usajili wa laini za simu kwa njia ya vidole na kuweka kitambulisho cha taifa kama kigezo muhimu.
Kwa sasa kampuni nyingi zinazotoa huduma za simu za mkononi zinatangaza usajili huo na tayari mwisho wa kutumia laini ambazo hazijasajiliwa kwa kitambulisho cha taifa imetangazwa kuwa ni Desemba 31.
Maeneo mengine ambayo bila kitambulisho cha taifa huwezi kupata huduma, ni pamoja na upatikanaji wa paspoti (hati ya kusafiria).
Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nayo imeweka kigezo kimojawapo ambacho mwanafunzi anahitajika kuwasilisha ili aweze kupata mkopo ni kitambulisho cha taifa.
Sehemu nyingine zinazohitaji vitambulisho ni wakati wa usajili wa kampuni kwa Wakala wa Usalili wa Kampuni (Brela), kupata leseni ya udereva, umiliki wa ardhi na hata ajira katika baadhi ya kampuni ya sekta binafsi.
Moris Jacob ambaye ni mkazi wa Chang’ombe, Dar es Salaam ni shuhuda mzuri kuhusu umuhimu wa kuwa na kitambulisho cha taifa baada ya hivi karibuni kutakiwa kukiwasilisha katika kampuni aliyoomba ajira mkoani Mbeya kama kigezo kimojawapo cha kumpatia ajira.
Moris alisema alijikuta akikosa ajira ya udereva kutokana na kukosa kitambulisho cha taifa.
“Nilipata nafasi ya ajira katika kiwanda kimoja huko mkoani Mbeya, nilifanya taratibu zote na nikasafiri kwenda Mbeya, lakini walinirudisha kwa kuwa sikuwa na kitambulisho cha uraia, hivi nimerudi na sasa hivi nimeanza mchakato wa kukitafuta japo naambiwa kukipata inachukua muda mrefu,” alisema Moris.
JAJI MKUU
Kuhusu watuhumiwa kupata dhamana kwa kutumia kitambulsho cha taifa, jambo hilo alilisema Jaji Mkuu kwa mara ya kwanza Julai 19, mwaka huu wakati wa mahafali ya 60 ya mawakili wapya katika Shule Kuu ya Sheria.
Wakati sasa akizielekeza mahakama kuanza kutumia vitambulisho hivyo, wakati huo alipendekeza kitambulisho hicho kitumike kwenye dhamana pasipo kutaka mshtakiwa kuonyesha mali.
Pendekezo hilo alilitoa ikiwa ni katika kushauri namna ya kutatua changamoto ya msongamano wa mahabusu magerezani kwa kulegeza masharti ya dhamana.
Kuhusu utekelezaji wa kutumia vitambulisho vya taifa kwenye dhamana, mwandishi mbobevu wa habari za mahakamani wa gazeti la Mtanzania, Kulwa Mzee, amesema tayari mahakimu wameanza kuruhusu kutumika kwenye kudhamini watuhumiwa.
Alisema tayari ameona zoezi hilo likifanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako yeye kwa muda mrefu amekuwa akiripoti kesi zinazoendelea.