29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Zaidi ya milioni moja waandamana Chile kumtaka rais wao ajiuzulu

SANTIAGO, CHILE

ZAIDI  ya watu milioni moja wameandamana nchini Chile katika maandamano makubwa zaidi ya kutaka mabadiliko ya kiuchumi na kujiuzulu kwa Rais Sebastian Pinera.

Waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera za maeneo yao na ya kitaifa, waliimba nyimbo maarufu za ukaidi kutoka enzi ya uongozi wa kidikteta wa Augusto Pinochet wa mwaka 1973-90.

Kuibuka kwa maandamano hayo katika taifa hilo ambalo kwa kawaida linaonekana kama thabiti zaidi katika Amerika ya Kusini, kumezua gumzo huku baadhi ya wachambuzi wakieleza hatua hiyo kama ni huenda ikalipeleka taifa hilo kukabiliana na ghasia mbaya zaidi katika muda wa miongo kadhaa.

Katika ukurasa wake wa twitter, gavana wa jimbo la Santiago Karla Rubilar aliitaja kuwa,” siku ya kihistoria” na kusifu,”maandamano ya amani…..yakiwakilisha ndoto ya Chile mpya.”

Rubilar amesema zaidi ya watu milioni moja walifanya maandamano kote nchini humo, huku baraza la mji wa Santiago likitaja idadi hiyo kuwa 820,000 pamoja na idadi ya polisi.

Katika muda wa wiki iliyopita, ghadhabu ya raia wa Chile ilisambaa kama maandamano dhidi ya mfumo wa kijamii na kiuchumi ambao wengi wanahisi kuwa umewatenga huku wakipata mapato ya chini na mafao, gharama ya juu ya matibabu na elimu na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini.

Pinera aliandika katika mtandao wa twitter kuwa; ” Maandamano haya makubwa, ya furaha na amani leo, ambapo raia wa Chile  wametaka serikali ya haki na ya kujali wananchi, yanafungua fursa muhimu za siku za baadaye na matumaini.”

Aliongeza kuwa, ” Sote tumesikia ujumbe huo. Sote tumebadilika. Kwa umoja na usaidizi kutoka kwa Mungu, tutaendelea katika njia ya kuifanya Chile kuwa bora kwa wote.”

Mapema wiki hii, Pinera aliomba radhi kwa kushindwa kufikiri iwapo kunaweza kuzuka maandamano na kutangaza mikakati kadhaa iliyowekwa kuwafidia watu kama vile kuongezwa kwa mafao ya kiwango cha chini na malipo ya ajira.

Pia alitangaza mpango wa kutamatisha hali ya hatari ya serikali isiyokuwa ya kawaida na kuondoa marufuku ya kutotoka nje usiku ijapokuwa hali hizo zinaendelea kwa siku ya saba sasa.

Katika ghasia zilizozuka hapo awali, vituo vya mabasi viliharibiwa, maduka ya jumla yalichomwa na kuibiwa na barabara kadhaa kuwekewa vizuizi.

Serikali ilipeleka maafisa 20,000 wa polisi na wanajeshi mjini Santiago waliotumia gesi na mabomba ya maji kuwatawanya waandamanaji.

Maafisa wa usalama wamelaumiwa kwa kwa vifo 19 vya waandamanaji.

Siku ya Alhamisi, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa unatuma kundi la maafisa wake kuchunguza madai hayo.

Visa vibaya na vya kukamatwa kwa watu vimepungua katika siku zilizopita ikilinganishwa na mwanzoni mwa vugu vugu hilo.

Waandamanaji walipokuwa wakipita nje ya Ikulu ya rais, walimtusi Pinera na jeshi la nchi hiyo.

Huku maandamano hayo yakionekana kuwa ya kupangwa, bado hayana viongozi wanaotambulika na yalichochewa zaidi kupitia mitandao ya kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles