25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanasaikolojia aleza kinachosumbua ndoa wasichana, wanaume

Elizabeth Hombo -Dar es salaam

MWANASAIKOLOJIA Christian Bwaya amezungumzia kwa undani hoja ya kuoa na kuolewa iliyoibuka kupitia msemo wa upepo wa kisulisuli.

Neno ‘upepo wa kisulisuli’ umepata umaarufu baada ya Mchungaji wa Kanisa la Mikocheni Assemblies of God, maarufu Mlima wa Moto, Getrude Lwakatare kuwataka  wasichana ambao hawajaolewa watoke mbele wakati wa ibada ili awaombee wapate waume wa kuwaoa.

Wakati akiomba Mchungaji Lwakatare aliamuru upepo wa kisulisuli uwapeleke wanaume kutoka pande zote kanisani hapo kwa ajili ya kuwaoa wasichana hao.

 “Wanaume kutoka Kaskazini, Magharibi, Mashariki waletwe na upepo wa kisulisuli, waletwe Mlima wa Moto waangalie wasichana wetu wawaoe,”alisema Mchungaji Lwakatare wakati akiwaombea wasichana hao.

Msemo huo wa Mchungaji Lwakatare umezalisha utani mwingi katika mitandao ya kijamii kiasi cha watu kuitumia kama mzaha na burudani huku wengine wakiibua mjadala wenye mtazamo tofauti kuhusu wasichana na suala zima la ndoa.

MTANZANIA Jumapili limefanya mahojiano na Mwanasaikolojia Christian Bwaya kuhusiana na suala zima la ndoa kwa pande zote wanaume na wanawake na jinsi linavyoonekana kutesa jamii.

Akizungumzia kwa upande wa wasichana  alisema kuna mambo mengi yanayochangia wasioelewe, lakini kubwa ni mtazamo wa jumla kwa wanaume kupenda sifa za nje kama urembo wa sura na maumbile ya mwili.

Alisema ingawa kuna ukweli kuwa wanaume wanavutiwa zaidi na vitu vinavyoonekana lakini wale waoaji wanaangalia zaidi ya maumbile na uzuri wa sura.

“Hapa ndipo wasichana wengi wanapopishana na waoaji. Kutumia muda mwingi kuonekana mrembo na wanasahau sifa nyingine muhimu kama nidhamu, heshima, kujituma, akili ya maisha na mambo kama hayo.

“Sisemi wanaume hawaangalii sura na umbile hapana. Lakini hayo hayatoshi kumshawishi mwanaume kuwa unafaa kuwa mke,”alisema.

Akiendelea kufafanua, Bwaya alisema jambo lingine ambalo linasababisha wasichana wengi wasiolewe ni kutokana na kujirahisisha kwa wanaume.

“Ingawa ni kweli wanaume kimaumbile wana tamaa ya mwili, lakini linapokuja suala la kuoa, mwanaume anatamani kuoa mwanamke anayejiheshimu na kwamba hapo ndipo wanawake wengi wanaposhindwa kuwaelewa wanaume.

“Mwanamume atakutamani, atataka kulala na wewe lakini akitaka kuoa anatafuta mtu anayejiheshimu. Mwanamke anayefikiri ukimridhisha mwanaume kingono atakuoa, atapishana na ndoa. Kama nilivyosema, ukimzoesha mwanaume ngono uwezekano wa kukuacha ni mkubwa,”alisema.

Mwanasaikolojia huyo, alisema sababu nyingine wasichana wengi hawakutani na watu sahihi na kwamba utakuta mwanamke ni mzuri na anajiheshimu lakini hakutani na watu wanaoweza kumuoa.

“Unakuta msichana akitoka kazini ni nyumbani lakini katika matukio yanayomkutanisha na wanaume haendi, sasa ataolewa na nani? Anatakiwa akutane na watu, awe na marafiki na watu wengi lakini jenga mipaka,”alisisitiza Bwaya.

Kutokana na hilo, aliwashauri wanawake kupandisha viwango vyao na kutengenza marafiki wengi lakini awe na mipaka na kwamba wasitumie miili yao kupata wanaume.

Akizungumzia kuhusu sababu za wanaume wengi kutooa, alisema wengi wao hawaoi kwa sababu ya woga.

Alisema kuna hofu ya aina mbili, kwanza ni ile ya majukumu kwamba akioa itakuwaje, akifunga ndoa itakuwaje akiyumba kiuchumi.

“Hilo ni kwa sababu wanaume wamekuzwa wakiamini kuwa wao ndio viongozi wa familia. Lazima wawe na uwezo wa kiuchumi kuhudumia familia. Katika mazingira ambayo hajakaa vizuri kiuchumi anajisikia fedheha kufikiria suala la kuoa,”alisema.

Alisema hofu ya pili ni kutokutabirika kwa wanawake na kwamba wanaume wanatafuta mwanamke atakayeweza kuwa mtii, mnyenyekevu na mwenye heshima.

“Sasa mara nyingi wakikutana na mwanamke anayeonekana kuwa na uwezo mkubwa, kasoma anajielewa, wanaume wengi wanakuwa na hofu ya kutawaliwa. Nadhani hilo nalo linachangia sana watu kushindwa kuoa.

“Kizazi chetu kina wanawake wanaojitambua mno kuliko ilivyopata kutokea huko nyuma. Kujitambua kwa wanawake ni tishio la kweli kweli kwa wanaume wengi waliolelewa wakiamini lazima umzidi mwanamke ili umtawale,”alisema.

Bwaya alisema mwanaume wa sasa hivi anahitaji kuwa na kitu cha ziada kuliko fedha na elimu kwa sababu hivyo vyote wanawake wengi wa kisasa wanavyo.

Alisema ili mwanaume wa sasa aheshimike, lazima awe na uwezo wa kumpenda mwanamke, kumlinda na kumtia moyo kusonga mbele kimaisha vinginevyo inakuwa vigumu mwanaume kupata mke wa kudumu kwenye ndoa.

“Lakini pia kingine kinachowasumbua wanaume ni tabia ya kuendekeza mno tamaa. Unapotembea na wanawake wengi unapata shida kuchagua. Ni ukweli wa kisiakolojia kuwa mwanaume akishalala na mwanamke ule msisimko unapungua. Kama hajitambui, anaweza kutembea na wanawake wengi warembo lakini haoni wa kuoa,”alisema.

Aliwataka wanaume kutumia muda mwingi kujitambua, kujifunza, kujenga urafiki na watu, kujijenga kiuchumi na sio kuendekeza tamaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles