32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Waliokamatwa Lindi kwa amri ya JPM wafika 99, warejesha sh milioni 436

Hadija Omary -Lindi

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURI), imesema viongozi wa Vyama vya Msingi (AMCOS) wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuwadhulumu wakulima imeongezeka kutoka 51 wa awali hadi 99, huku fedha zilizozulumiwa zikiongezeka kutoka Sh milioni 436.869 hadi Sh bilioni 1.236.

Ukamatwaji wa viongozi hao ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Oktoba 10 mwaka huu  wakati  wa mkutano wa hadhara aliofanya wilayani  Ruangwa Mkoa wa Lindi.

Rais aliagiza Takukuru na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuhakikisha AMCOS  zinazodaiwa na wakulima wa ufuta, viongozi wake wasakwe wawalipe wakulima hao fedha zao kabla ya msimu mpya kuanza.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Generali John Mbungo, alisema kati ya waliokamatwa wamesharejesha Sh milioni 255.598.

Alisema ongezeko la viongozi wa AMCOS  wanaoshikiliwa limetokana na taasisi yao kuendelea kufanya msako katika vyama hivyo.

” Ingawa taarifa iliyokabidhiwa Takukuru na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ilikuwa inaonyesha wakulima wa ufuta wamedhurumiwa Sh milioni 436.869 na vyama 10 vya msingi,  uchunguzi na ufuatiliaji  uliofanywa na Takukuru ulibaini kuwepo kwa vyama 31 vya msingi ambavyo vimedhulumu wakulima  wa ufuta Sh bilioni 1.236″ alisema Mbungo

Alisema tokea zoezi hilo la kuwakamata viongozi hao lianze Oktoba 16 hadi Oktoba 19, Sh milioni 255.598  zimerejeshwa katika Ofisi ya Takukuru na zitaanza kulipwa kwa wakulima kwa utaratibu utakaopangwa. 

Mbungo pia alisema katika kuhakikisha wakulima waliozulumiwa fedha zao wanapata haki yao, Takukuru imeanza kutambua mali za viongozi hao wa AMCOS wanaodaiwa ili ziwe dhamana ya madeni wanayodaiwa na wakishindwa kulipa kwa muda waliokubaliana mali hizo ziuzwe kulipa madeni ya wakulima.

Mbungo pia alitoa rai kwa viongozi wote wa vyama vya ushirika nchini vinavyodaiwa na wakulima viwalipe wakulima hao haraka kabla ya Takukuru haijawafikia kwani zoezi hilo  ni endelevu na hakutakuwa na chama cha ushirika kinachodaiwa kitakachobaki salama.

Siku moja baada ya agizo hilo la Rais, Bashe alimweleza Rais Magufuli kwamba ma tayari ameshaagiza kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya ushirika waliokula fedha za wakulima na wameshawekwa ndani, ambao hawataachiwa hadi fedha zilizopotea zipatikane.

Kwa hatua hiyo, Rais Magufuli aliingilia kati huku akimsifu Bashe kuwa ndio aina ya viongozi anaowataka na alitaka kujua jina la kiongozi mwingine wa Amcos ambaye alikuwa bado hajakamatwa, na alipoelezwa kuwa anaitwa Seif Misele, aliagiza akamatwe haraka na asiachiwe hadi fedha zitakapopatikana. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles