Nyumba 400, magari 200 yaunganishiwa gesi ya Mtwara

0
735

Gustaph Haule -Pwani

ZAIDI ya nyumba 400 zilizopo katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani zinatarajia kunufaika na huduma ya gesi asilia inayotolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).

Mtaalamu mwandamizi wa masuala ya Petroli(Geologist) kutoka TPDC, Simon Zabron alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika  maonyesho ya bidhaa za viwandani yanayoendelea kufanyika kwenye viwanja vya Mkuu wa Mkoa wa Pwani vilivyopo Mjini Kibaha.

Zabron, alisema mradi wa kusambaza gesi asilia majumbani unaendelea vizuri na kwamba ifikapo Novemba mwaka huu tayari nyumba 400 zitakuwa zimefikiwa ambapo kati ya hizo nyumba 125 kutoka Mkoa wa Mtwara na nyingine zilizobaki zipo katika Jiji la Dar es Salaam.

“Mradi wa kusambaza gesi asilia unakwenda vizuri ambapo kwasasa tunatarajia nyumba 400 kunufaika ifikapo Novemba mwaka huu lakini zoezi hilo litaendele kutekelezwa kwakuwa lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa ,”alisema Zabron.

Mbali na nyumba hizo Zabron,alisema tayari hadi sasa viwanda 45 vinafanya uzalishaji wake kwa kutumia gesi inayosambazwa na TPDC na miongoni mwa viwanda hivyo ni kiwanda cha Dangote kilichopo Mkoani Mtwara na Godwell kilichopo Mkiu, Mkuranga Pwani.

Alisema, viwanda vingine vipya vitakavyonufaika na mradi huo ni kiwanda cha Lodhia ambapo hatahivyo alisema TPDC wapo tayari kutoa huduma ya gesi kwenye viwanda vyote vilivyopo katika Mikoa ya Mtwara na Dar es Salaam kwakuwa miundombinu yake imekamilika.

Kuhusu huduma za gesi kwenye magari, Zabron alisema kuwa mpaka sasa tayari magari 200 yanatumia gesi asilia nchini na kwamba magari yanayounganishwa na huduma hiyo ni yale yaliyokuwa kwenye mfumo wa kutumia Petroli.

Alisema, mradi wa magari kuunganisha gesi ulianza miaka saba iliyopita lakini ulikuwa unasuasua kutokana na mwamko mdogo lakini kwasasa hamasa imekuwa kubwa na watu wengi wanajitokeza kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Alisema wamiliki wa viwanda waliopo Dar es Salaam na Mtwara wanaweza kupata huduma ya gesi muda wowote wanapohitaji  huku akihamasisha watu wajenge viwanda kwa wingi ili wapate huduma ya gesi kirahisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here