MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
KATIKA kuthibitisha kuwa imepania kupindua meza, kikosi cha timu ya Taifa Tanzania ‘ Taifa Stars’, tayari kimetua Sudan, kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya
Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani(Chan), utakaopigwa Ijumaa hii jijini Khartoum.
Timu hizo zilipoumana katika mchezo wa kwanza uliochezwa Septemba 22, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Sudan iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stars.
Ili kuishinda Sudan na kutinga hatua ya makundi, Stars itatakiwa kupata ushindi wa kuanzia mabao 2-0, zitakaporudiana kesho kutwa.
Kikosi cha Stars kiliondoka Kigali juzi usiku kwenda Khartoum, baada ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Rwanda uliochezwa Uwanja wa Amahoro na kumalizika kwa suluhu.
Mchezo huo huo wa kujipima ubavu ulikuwa kukidhi matakwa ya Kalenda ya
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Mchezo wa marudiano kati ya Stars na Sudan utakaopigwa Uwanja wa Omdurman, wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 65,000.
Sababu ya kikosi
cha Stars kuunganisha moja kwa moja Sudan, zinalengwa na kuwapa muda wa kuzoea
hali ya hewa wachezaji wa kikosi hicho.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wao na Rwanda juzi, Kaimu Kocha Mkuu wa Stars,
Etienne Ndayiragije alisema aliridhishwa na suluhu waliyoipata na kudai kuwa,
mchezo dhidi ya Rwanda ulikuwa kipimo
sahihi kwao .
“Nashukuru kwa mchezo kumalizika salama, nimeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wangu, nakiri kwamba tulipata mtihani sahihi kulingana na kazi iliyo mbele yetu.
“Mchezo huu utatusadia sana katika maandalizi yetu kuelekea mechi ya marudiano na Sudan, kuna vitu vichache vya kufanyia kazi na bado tuna muda wa kurekebisha, lakini vijana walicheza kwa kufuata maelekezo yangu, nimefurahishwa na hali hiyo,” alisema kocha huyo raia wa Burundi.