Simba msako wahamia kwa Warundi

0
582

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

BAADA ya juzi kulipa kisasi kwa Mashujaa FC, kikosi cha Simba kitashuka dimbani leo kuivaa Aigle Noir ya Burundi, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki, utakaochezwa  Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Huo utakuwa mchezo wa tatu wa kirafiki kwa kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi, baada ya kuitungua Bandari ya Kenya bao 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na juzi kupata ushindi kama huo dhidi ya Mashujaa.

Simba inaendelea kutumia kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi Kuu, kupisha michezo ya kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kujiweka fiti kwa kucheza mechi za kirafiki.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara , wananoa makucha kabla ya kuikabili Azam FC,  katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa Oktoba 23, mwaka huu  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Aigle kwa upande wake itautumia mchezo huo kujiweka tayari kwa muendelezo wa Ligi Kuu Burundi,  baada ya kukamilika kwa kalenda Fifa.

Hiyo si ya mara kwanza kwa Aigle kucheza dhidi ya timu za Tanzania, iliwahi kuumana na Namungo, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar  na Azam  ilipofanya  ziara ya kimichezo ya maandalizi ya msimu mpya.

Akizungumza na MTANZANIA  jana, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema watatumia mchezo huo kujiweka sawa kabla ya kuendeleza harakati zao za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu.

“Tunashukuru kwa kumaliza mchezo salama dhidi ya Mashujaa, ushindi si kitu kwetu, bali mwalimu alitaka kukiweka tayari kikosi chake kwa mapambano ya ligi, ndiyo maana alitumia sehemu kubwa ya wachezaji wa kikosi B na timu bao ilifanya vizuri.

“Tutamaliza ziara yetu Kigoma kwa kucheza  dhidi ya Aigle Noir, tunashukuru tumepata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wetu ambao hawajawahi kuiona timu yao ikicheza mkoani hapa kwa miaka 15 iliyopita,” alisema Rweyemamu.  

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here