CHRISTOPHER MSEKENA
MWANZONI mwa mwaka 2013, aliyekuwa mhifadhi mkuu wa
Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Erastus Lufungulo, alimkabidhi staa wa Bongo Fleva,
Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, cheti cha uthibitisho wa kufika kileleni.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Lady Jay Dee
aliyeongozana na meneja wake wa zamani, Gardner G Habash kufika katika kilele
cha Uhuru cha mlima huo, mita 5,895 kutoka usawa
wa bahari.
Miaka
sita mbele mastaa mbalimbali kama vile Hamis Mwinjuma ‘Mwana Fa’, mwigizaji
nyota Kulwa Kikumba ‘Dude’, meneja wa Shilole Mx Carter, Queen Elizabeth Makune
na mzalendo halisi ambaye ni mdau wa muziki wa Gospo, Ikuzi Kicheko
wamefanikiwa kufika kwenye kilele hicho.
Kupitia
kampeni ya Twenzetu Kileleni, wasanii,
wanahabari na watu wengine zaidi ya 100 walianza safari ya kuelekea kileleni
Jumamosi iliyopita katika safari iliyodumu kwa siku sita.
Mastaa
kibao walishiriki kwenye kampeni hiyo ya kuhamasisha utalii wa ndani. Miongoni
mwao ni mwanamuziki Diamond Platnumz na meneja wake, Babu Tale, waigizaji Steve
Nyerere, Single Mtambalike, JB, Ebitoke, Amini na AT.
Wengine
ni Mwarabu Fighter, Husna Sajent, Dogo Janja, Mheshimiwa Temba, Davina, Cathy
Rupia, Maya Mrisho, Mariam Ismail na wengi wengine.
Ila
kati ya hao wote waliofanikiwa kufika kilele cha Uhuru ni hao wachache niliowataja
hapo juu huku wengi wakiishia kwenye vituo vya chini kama vile kituo cha kwanza
cha Mandara, cha pili cha Horombo na Kibo Huts.
Miongoni
mwa wasanii waliokomaa kiume ni Ebitoke ambaye alikuwa msichana pekee
aliyepanda urefu mkubwa zaidi mpaka kituo cha Gilman’s ambacho ni mita 5,685
kutoka usawa wa bahari.
Staa
mwingine aliyekomaa kiume ni AT na Shetta ambaye licha ya kuwa na safari ngumu walidhamiria
kufika kwenye kilele cha Uhuru na hatimaye wakaishia kituo cha Gilman’s.
Katika
pongezi za Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla kwa Shetta
alisema: “Ilikuwa safari ngumu sana kwa
Shetta lakini alitaka lazima afike kileleni na alifika kituo cha Gilman’s ambacho ni mita 210 kutoka kilele cha Uhuru
na ndiyo sehemu ngumu zaidi kufika, ukiwa hapo unakiona kibao cha Uhuru Peak
kiurahisi kabisa lakini kufika sasa ni ngumu na watu wengi hukwama kufika
sababu ya ugumu wake.”
Akizungumza na Swaggaz, Ikuzi Kicheko ambaye alikuwa
miongoni mwa watu wa kwanza kufika kwenye kilele cha Uhuru anasema: “ Kwanza
kabisa safari ni ngumu siyo safari ya kitoto, harafu tulipokuwa tunaanza
kupanda mlima kila mtu alikuwa na picha yake ya mlima ulivyo, stori nyingi
ambazo tulikuwa tunazisikiliza zilikuwa siyo za ukweli, tulifikiri tunaanza
kupanda mlima chini mpaka kileleni lakini kumbe mlima ni mkubwa sana, kuna
safari ya vituo vitatu ambavyo navyo vina changamoto sababu ya umbali.
“Pili wengi walikuwa wanapanda mlima kwa spidi kali
kumbe mlima una sheria zake na wengi sheria zake tulikuwa hatufati, inatakiwa
uende taratibu kwa hatua na kila baada ya hatua kadhaa unywe maji sababu
inakuwa kama dawa ya kukupa nguvu, tunamshukuru Mungu tumeweza kupanda na kufika.”
Aliongeza kuwa : “Tatu hali ya hewa ni ngumu sana,
hali ya hewa ya kule ni tofauti na hii ya kwetu huku chini, kule oksijeni ni ndogo harafu ni nzito, kila unavyopanda
mlima unaangalia chini unaona mawingu tu, huoni nyumba wala nini, binafsi najipanga
nirudi kupanda tena mlima sababu
nimepata uzoefu, nataka kuweka historia kama watu wengine waliopanda mlima kwa
siku moja, wengine kwa saa nane, mimi nategemea kupanda mlima kwa muda mfupi.”
Katika safari hiyo iliambatana na vituko kibao ikiwa
ni pamoja na Steve Nyerere kutamba kutumia mfumo wa mpira wa miguu wa 4 4 2
kupanda na kushuka kwenye mlima huo lakini akaishia kituo cha kwanza akiwa hoi
bin taabani huku Diamond akishindwa kufika kutokana na majukumu mengine.