Mwana Fa, Dude, Ikuzi walivyotoboa kileleni

0
1182

CHRISTOPHER MSEKENA

MWANZONI mwa mwaka 2013, aliyekuwa mhifadhi mkuu wa Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Erastus Lufungulo, alimkabidhi staa wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, cheti cha uthibitisho wa kufika kileleni.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Lady Jay Dee aliyeongozana na meneja wake wa zamani, Gardner G Habash kufika katika kilele cha Uhuru cha mlima huo, mita 5,895 kutoka usawa wa  bahari.

Miaka sita mbele mastaa mbalimbali kama vile Hamis Mwinjuma ‘Mwana Fa’, mwigizaji nyota Kulwa Kikumba ‘Dude’, meneja wa Shilole Mx Carter, Queen Elizabeth Makune na mzalendo halisi ambaye ni mdau wa muziki wa Gospo, Ikuzi Kicheko wamefanikiwa kufika kwenye kilele hicho.

Kupitia kampeni ya  Twenzetu Kileleni, wasanii, wanahabari na watu wengine zaidi ya 100 walianza safari ya kuelekea kileleni Jumamosi iliyopita katika safari iliyodumu kwa siku sita.

Mastaa kibao walishiriki kwenye kampeni hiyo ya kuhamasisha utalii wa ndani. Miongoni mwao ni mwanamuziki Diamond Platnumz na meneja wake, Babu Tale, waigizaji Steve Nyerere, Single Mtambalike, JB, Ebitoke, Amini na AT.

Wengine ni Mwarabu Fighter, Husna Sajent, Dogo Janja, Mheshimiwa Temba, Davina, Cathy Rupia, Maya Mrisho, Mariam Ismail na wengi wengine.

Ila kati ya hao wote waliofanikiwa kufika kilele cha Uhuru ni hao wachache niliowataja hapo juu huku wengi wakiishia kwenye vituo vya chini kama vile kituo cha kwanza cha Mandara, cha pili cha Horombo na Kibo Huts.

Miongoni mwa wasanii waliokomaa kiume ni Ebitoke ambaye alikuwa msichana pekee aliyepanda urefu mkubwa zaidi mpaka kituo cha Gilman’s ambacho ni mita 5,685 kutoka usawa wa bahari.

Staa mwingine aliyekomaa kiume ni AT na Shetta ambaye licha ya kuwa na safari ngumu walidhamiria kufika kwenye kilele cha Uhuru na hatimaye wakaishia kituo cha Gilman’s.

Katika pongezi za Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla kwa Shetta alisema: “Ilikuwa safari ngumu sana kwa Shetta lakini alitaka lazima afike kileleni na alifika kituo cha Gilman’s  ambacho ni mita 210 kutoka kilele cha Uhuru na ndiyo sehemu ngumu zaidi kufika, ukiwa hapo unakiona kibao cha Uhuru Peak kiurahisi kabisa lakini kufika sasa ni ngumu na watu wengi hukwama kufika sababu ya ugumu wake.”

Akizungumza na Swaggaz, Ikuzi Kicheko ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika kwenye kilele cha Uhuru anasema: “ Kwanza kabisa safari ni ngumu siyo safari ya kitoto, harafu tulipokuwa tunaanza kupanda mlima kila mtu alikuwa na picha yake ya mlima ulivyo, stori nyingi ambazo tulikuwa tunazisikiliza zilikuwa siyo za ukweli, tulifikiri tunaanza kupanda mlima chini mpaka kileleni lakini kumbe mlima ni mkubwa sana, kuna safari ya vituo vitatu ambavyo navyo vina changamoto sababu ya umbali.

“Pili wengi walikuwa wanapanda mlima kwa spidi kali kumbe mlima una sheria zake na wengi sheria zake tulikuwa hatufati, inatakiwa uende taratibu kwa hatua na kila baada ya hatua kadhaa unywe maji sababu inakuwa kama dawa ya kukupa nguvu, tunamshukuru Mungu tumeweza kupanda na kufika.”

Aliongeza kuwa : “Tatu hali ya hewa ni ngumu sana, hali ya hewa ya kule ni tofauti na hii ya kwetu huku chini, kule oksijeni  ni ndogo harafu ni nzito, kila unavyopanda mlima unaangalia chini unaona mawingu tu, huoni nyumba wala nini, binafsi najipanga nirudi kupanda tena  mlima sababu nimepata uzoefu, nataka kuweka historia kama watu wengine waliopanda mlima kwa siku moja, wengine kwa saa nane, mimi nategemea kupanda mlima kwa muda mfupi.”

Katika safari hiyo iliambatana na vituko kibao ikiwa ni pamoja na Steve Nyerere kutamba kutumia mfumo wa mpira wa miguu wa 4 4 2 kupanda na kushuka kwenye mlima huo lakini akaishia kituo cha kwanza akiwa hoi bin taabani huku Diamond akishindwa kufika kutokana na majukumu mengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here