25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Moto wa Majaliwa wahamia Singida

Mwandishi wetu-Singida      

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amempa siku tatu Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya ya Itigi, Optatus Likiliwike, kurejesha Sh milioni 1.6 ambazo alijilipa posho kinyume cha utaratibu.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Manyoni ambao wanajumuisha Halmashauri za Wilaya za Itigi na Manyoni.

 â€œKabla sijamaliza ziara tarehe 7, nataka nione pay in slip kuthibitisha kuwa fedha hiyo imerudishwa. Adhabu yako kaweke fedha benki, niione hiyo pay in slip kabla sijaondoka,” alisema Majaliwa.

“Wewe si ndiye Otto au Optatus? Mwezi Julai ulilipwa posho ya safari ili uende Dodoma kukamilisha mahesabu ya bajeti lakini hukwenda. Taratibu za fedha zinasema ukitumia fedha, urejeshe, wewe ulifanyaje?,” alihoji  Majaliwa.

 â€œNilichukua fedha lakini kutokana na majukumu mengi niliyo nayo, sikwenda nikawa naenda wikiendi na kuna kazi nyingine haikuwa ni lazima niwepo Dodoma,” alijibu Likiliwike.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alimtaka ofisa huyo arejeshe Sh. milioni 196 za ujenzi wa ofisi ya halmashauri ambazo zimetumika kinyume na zilivyopangwa.

“Hizi fedha zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi. Hizi ni fedha za retention, ni nani alikiuka maelekezo na kuamua kuzitumia kwa kazi nyingine?” Majaliwa alijibiwa kwamba ni Mkurugenzi na Mweka hazina waliokuwepo kabla yake.

Majaliwa alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, John Mgalula ambaye aliteuliwa wiki iliyopita, asimamie marejesho ya posho za Likiliwike na marejesho ya sh. milioni 196 ambazo mweka hazina huyo ameahidi kuwa Halmashauri yake imetenga Sh. milioni 70 ili zirejeshwe kila mwaka.

Alisema wanapaswa kutenga fedha zaidi ili fedha hiyo iweze kurejeshwa haraka kwa Wakala wa Majengo nchini (TBA) ambaye ni mkandarasi wa jengo la ofisi za Halmashauri hiyo.

Naye BwOptatus Otto Likiliwike alisema fedha zinazodaiwa kutumika, zilikuwa zimetumwa na Hazina kwa ajili ya ujenzi wa ofisi lakini zililazimika kuchotwa na uongozi uliopita ili zitumike kuweka miundombinu ya kuanzisha Halmashauri mpya ya Itigi.

Alisema waliohusika ukiukwaji huo ni Mkurugenzi aliyepita, Pius Luhende na Mweka Hazina aliyepita Charles Mnamba. Hata hivyo, alikiri fedha hizo hazikuombewa kibali cha matumizi.

Akiweka jiwe la msingi kwenye jengo hilo, Majaliwa alisema anaweka jiwe hilo kwa sababu ameridhishwa na maelezo ya Meneja wa TBA kuhusu ujenzi wa jengo hilo.

Awali, alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Charles Fussi ahakikishe anarejesha mkopo wa Sh. milioni 100 kutoka benki ya CRDB ambazo walikopeshwa madiwani, wakarejesha kiasi lakini halmashuri haijazipeleka benki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles