Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka amesema kuwa malipo yote ya wakulima wa pamba katika msimu ujao wa mauzo mwakani, yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia benki na kampuni za simu ikiwemo TTCL.
Mtaka amesema hayo leo kwenye mkutano uliowahusisha viongozi wa Amcos uliokuwa na lengo la kuelezea malipo ya wakulima wa pamba kulipwa kupitia T-Pesa uliofanyikia mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
Amesema kuwa moja ya kampuni ya simu ambayo wakulima wataitumia kupata pesa zao ni TTCL kupitia T-Pesa, ambapo amesema kampuni hiyo imejitokeza ikiwa ya kwanza kutumia fursa hiyo na wakulima wanatakiwa kununua laini zake.
“Wakulima lazima wafahamu kuwa serikali tayari imetangaza kuwa malipo hayatafanyika kwa mkono tena baada ya msimu wa mwaka huu, kuanzia msimu ujao malipo yote yatafanyikia benki na mkulima atapata pesa zake akiwa nyumbani kupitia T-Pesa,” amesema Mtaka.
Aidha amewataka wakulima kuchukua laini hizo kwani mfumo wa malipo utabadilika huku akiwaagiza viongozi wa Amcos kuhakikisha wanawaeleza wakulima kwa ajili ya kujiandaa.
Awali akiongea katika mkutano huo Mkurugenzi wa TTCL Waziri Kindamba alisema kampuni hiyo imekuja na mfumo huo ili wakulima wa pamba waepuke matatizo ya fedha zao kuibiwa kupitia viongozi wa vyama vya ushirika ambao siyo waaminifu ikiwemo usalama wa pesa zao.