NA VICTOR BARIETY, GEITA
MAUAJI ya kinyama ambayo yanahusishwa na imani za kishirikina yameanza kurejea mkoani Geita, baada ya watu wanne wa familia moja wakazi wa kijiji cha Bugalama wilayani Geita kuuawa.
Watu ambao majina yao hajatambuliwa mara moja, wameuawa kwa kuchinjwa shingo kama kuku.
Waliouawa katika tukio hilo lililotokea Desemba Mosi, ni wanawake watatu na mtoto mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,Latson Mponjoli alipoulizwa jana alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Mponjoli alisema hivi karibuni mkazi wa kijiji hicho, Samweli Masibo alifariki dunia,baada ya kuugua maradhi ya kawaida.
Alisema marehemu Masibo alikuwa na wake watatu na siku chache baada ya kufariki dunia alianza kuonekana kwa njia za kishirikina nyumbani kwa mke wa pili ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Wanasema eti marehemu alikuwa anaonekana usiku nyumbani kwa mke wa pili na kwamba hakufariki,  bali aliuawa kishirikina masuala ambayo sisi hatuwezi kuyathibitisha’’alisema Kamanda Mponjoli.
Alisema  jana (juzi) wakati familia hiyo ikiwa inaota moto usiku lilitokea kundi la watu ambao hawakujulikana mara moja, wakiwa na silaha za jadi na kuanza kushambulia kila mtu aliyekuwa mbele yao na kusababisha vifo hivyo.
‘’Kwa kweli hili tukio linasikitisha,wameuawa kinyama wametenganishwa vichwa na kiwiliwili…polisi tumeanza kuchukua hatua.Tunaomba mtuvumilie kesho (leo) tutawapa majina yote ya marehemu,’’alisema mponjoli.