25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jela miaka 40 kwa kukutwa na dawa za kulevya

KULWA MZEE –dar es salaam

MFANYABIASHARA Waziri Mizoge, aliyekutwa na dawa za kulevya gramu 2193.1 nyumba ya kulala wageni Tunduma, amehukumiwa kwenda jela miaka 40 na kulipa faini zaidi ya Sh milioni 200.

Mizoge alihukumiwa juzi na Mahakama Kuu Mkoani Songwe mbele ya Jaji Dk. Adam Mambi, baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi wa Jamhuri kwamba alifanya makosa hayo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Achiles Mulisa alidai mshtakiwa alikamatwa Mei 4 mwaka 2012 katika nyumba ya kulala wageni inayoitwa Nice Shirez, Tunduma akiwa na heroine gramu 1645.89 na mchanganyiko wa heroine na cocaine gramu 547.21.

Baada Jamhuri kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka, mahakama ilimtia hatiani na kumuhukumu kwa makosa yote mawili.

Katika kosa la kwanza la kukutwa na gramu 1645.89, mshtakiwa alipewa adhabu ya kwenda jela miaka 20 na kulipa faini ya Sh 73,873,350.

Kosa la pili la kukutwa na mchanganyiko wa heroine na cocaine, amehukumiwa kwenda jela miaka 20 na kulipa faini ya Sh 197,080,450.

Mshtakiwa alikutwa na gramu 2193.1 za dawa za kulevya na anatakiwa kwenda jela miaka 40 na kulipa faini ya Sh 270,953,800 kwa makosa yote. Mahakama imeamuru dawa ziteketezwe.

Wakati huo huo, Mwinyi Rajabu Mkazi wa Magomeni na Ally Hamad Mkazi wa Mbezi Luis, Dar es Salaam wamehukumiwa kwenda jela kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 63.155.

Washtakiwa hao walihukumiwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, mbele ya Jaji Lilian Mashaka.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Saraji Ebora akisaidiana na Wakili wa Serikali, Kauli Makasi, walidai kwa nyakati tofauti kuwa washtakiwa walikamatwa Novemba 7 mwaka juzi maeneo ya mpaka wa Kalambo mkoani Mtwara.

Washtakiwa walikamatwa wakiwa wameficha dawa hizo katika gari aina ya Toyota Alphard yenye namba za usajili T 499 DCI.

Mahakama iliwatia hatiani baada ya kuona mashtaka dhidi yao yamethibitishwa bila kuacha shaka.

Washtakiwa wamehukumiwa kwenda jela miaka 20 na mahakama imeamuru gari lililotumika kusafirisha dawa hizo litaifishwe na kuwa mali ya Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles