Gurian Adolf -Kalambo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kupitia Idara ya Mifugo na Uvuvi, imeanza operesheni maalumu ya kuua mbwa baada ya kujitokeza wimbi la watu kufariki dunia kwa kuumwa na mnyama huyo.
Operesheni hiyo ilianza rasmi juzi baada ya mbwa mmoja aliyesadikiwa kuwa na kichaa, kung’ata watoto 14 katika vijiji vya Keleni na Matai asilia, pamoja na watu wazima watatu katika Kijiji cha Kisungamile na mmoja katika Kijiji cha Santa Maria ambaye alifariki dunia.
Kutokana na matukio hayo, wananchi walilazimika kuiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia kwa kuwapatia chanjo mbwa wote na kuwaua wale ambao wamekuwa wakizurura ovyo bila uangalizi maalumu.
“Tunaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwachanja mbwa wote pamoja na kusogeza huduma ya chanjo ya kuzuia kichaa cha mbwa kwenye vituo vya afya na zahanati zote, badala ya kufuata huduma hiyo mjini Sumbawanga kutokana na baadhi ya watu kuumwa na mbwa hao na wamekuwa wakichelewa kupata matibabu na hatimaye kupoteza maisha,” alisema John Futakamba ambaye ni mkazi wa Matai asilia.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Santa Maria, Ofisa Mifugo na Uvuvi wilayani humo, Wilbroad Kansapa alisema wilaya hiyo ina jumla ya mbwa 6,360.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, amewasiliana na Mganga Mkuu wa Wilaya, kuhakikisha dawa za kuwatibu watu ambao wamekuwa wakiumwa na mbwa zinapatikana vituo vyote vya afya na zahanati.
Pia alisema Idara ya Mifugo wilayani humo, imeamua kuanzisha operesheni maalumu ya kuwapiga risasi na kuwaua mbwa wote wanaozurura bila uangalizi maalumu kwa kuwa hawana matunzo.
Aliwataka wananchi wote wanaofuga mbwa kuwapeleka kuchanjwa pindi tangazo linapotolewa na kwamba lazima wafungwe kuanzia saa kumi na moja alfajiri na kufunguliwa saa sita usiku, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaokaidi sheria hiyo.