Tunu Nassor -Dar es salaam
MANISPAA ya Ilala imefanikiwa kuongeza watumiaji wa njia za uzazi wa mpango kutoka 69,185 mwaka juzi hadi 81,198 mwaka jana.
Akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa afya jana, Mratibu wa Huduma za Uzazi wa Mpango Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, Edith Kijazi, alisema ndani ya mwaka mmoja wamefanikiwa kuongeza watumiaji 12,013.
Edith alisema ongezeko hilo limetokana na kupata udhamini kutoka Taasisi ya JHPIEGO kupitia mradi wa TCI Tupange Pamoja unaotekelezwa na manispaa hiyo.
“Tafiti zinaonyesha matumizi sahihi ya njia ya uzazi wa mpango yanapunguza vifo kwa asilimia 40, tunaendelea kuwafikia wateja wengi zaidi,” alisema.
Alisema halmashauri hiyo inatoa huduma ya uzazi wa mpango na huduma rafiki kwa vijana kwa ushirikiano wa wadau.
“Lengo kuu kuwafikia wahitaji wa huduma ya uzazi wa mpango ambao hawajafikiwa kwa dhumuni la kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga vitokanavyo na uzazi,” alisema.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, aliwashauri mabalozi wa uzazi wa mpango kutumia mifumo ya mawasiliano ya mtandao ili kuwafikia watu wengi zaidi.
“Suala la afya ya uzazi ni makubaliano baina ya baba na mama, naomba mabalozi wa uzazi wa mpango kutoa elimu kwa mfumo wa mawasiliano ya kisasa ili jamii wapate elimu mapema,” alisema.
Alisema mkakati wa uzazi wa mpango, ukiingizwa kwenye Tehama lengo litatimia kwa kuwa wananchi watapata taarifa.