32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Zahera aisukia mkakati Zesco

Mwamvita Mtanda

KUELEKEA mchezo wa marudiano wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema mipango yake ni ‘bab kubwa’ kuhakikisha wanashinda ugenini na kutinga hatua ya makundi.

Kauli ya Zahera raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) inakuja licha ya Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Zesco katika mchezo wa kwanza uliochezwa hivi karibuni katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Yanga imekuwa na historia nzuri tangu kuanza kwa michuano hiyo, kwamba haijawahi kupoteza ugenini, jambo linalowapa matumaini mashabiki wake kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupata ushindi katika mechi hiyo ya marudiano kule Zambia.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Zahera alisema anajipanga upya, akihakikisha anarekebisha makosa ambayo yalitokea katika mechi iliyopita, akiahidi kuipanga vyema safu yake ya ushambuliaji.

Alisema mazoezi ambayo anawapa wachezaji wake kwa sasa ni ya kujilinda na kushambulia zaidi ili kupata mabao wakiwa ugenini. “Hii michuano unatakiwa ucheze na akili zaidi. Sasa hivi nafanya kazi kubwa ya kuwapa mbinu mabeki, namna ya kukaba na washambuliaji namna ya kushambulia na kujuilinda. Ninaamini tutakwenda kufanikiwa juu ya hili.

“Kufunga tutafunga, hajalishi tutafunga kwa namna gani, lakini kinachotakiwa zaidi ni ushindi,” alisema Zahera.

Akiizungumzia rekodi yao hiyo ya ugenini, mkufunzi huyo alisema: “Ukiona timu inafanya vizuri ugenini kuliko nyumbani, ujue uzoefu wake upo kimataifa zaidi, hivyo lazima tuwe na matumaini kuwa tutashinda.”

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema anajipanga kwenda Zambia Septemba 23, mwaka huu, ili kuweka sawa mipango ya ushindi.

Alisema kwa kuwa lengo lao ni kufanikisha kuingia katika hatua ya makundi, lazima wafanye jitihada zote kuhakikisha wanashinda. “Mipango lazima iwepo ya nje na ndani ya uwanja na haitaweza kufanikiwa ikiwa tutachelewa kufika Zambia. Mimi nitatangulia ili kuweka mambo sawa,” alisema Mwakalebela.

Yanga inatarajia kuondoka Septemba 24, ikielezwa kuwa wataingia dimbani Septemba 26, mwaka huu, kukabiliana na wenyeji wao hao, Zesco.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles