Mexime amnyima usingizi Mbelgiji

0
605

Theresia Gasper -Dar es salaam

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amesema anafahamu wanaenda kukutana na timu ambayo iliwafunga mechi zote mbili katika msimu uliopita, hivyo lazima wajiandae vizuri.

Wekundu wa Msimbazi wanajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, unaotarajiwa kuchezwa Septemba 26 mwaka huu, Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Kagera Sugar chini ya kocha mzawa, Meck Mexime, ni timu pekee ambayo msimu uliopita iliweza kuifunga Simba mechi zote mbili, ambapo mzunguko wa kwanza waliwapa kichapo cha mabao 2-1 pale Kaitaba, kabla ya kuwafunga tena 1-0 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kuelekea mchezo huo, Wekundu wa Msimbazi wameshinda mechi zao zote mbili; dhidi ya JKT Tanzania waliposhinda mabao 3-1, kabla ya kuirarua Mtibwa Sugar mabao 2-1.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Aussems, alisema bado wana muda mrefu wa kujiandaa na lazima wawe na tahadhari kubwa, ikiwamo kuwafuatilia wapinzani wao hao.

“Tumeanza mazoezi leo (jana) baada ya kupata mapumziko mafupi, hivyo tutaendelea kufanya kwa umakini kwani tunaenda kukutana na timu ambayo msimu uliopita ilitufunga katika mechi zote mbili,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mbelgiji huyo alisema mipango ni ile ile ya kupata pointi tatu kwa kila mechi ili kujiwekea vizuri katika malengo yao ya kutwaa ubingwa kwa mara nyingine.

Aussems alisema wataangalia uwezekano wa kupata mechi yoyote ya kirafiki, akiongeza kuwa kwa sasa wachezaji wake wamerejea dimbani isipokuwa John Bocco ambaye ni majeruhi.

Simba wamejichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, wakiwa wamejikusanyia pointi sita katika mechi mbili walizocheza, sawa na Lipuli FC na Namungo FC, timu hizo zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here