33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi kesi ya mauaji waruhusiwa kujiandaa mtihani wakiwa gerezani

Nyemo Malecela -Kagera

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Katoro Islamic ya mkoani Kagera, wanaotuhumiwa katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi mwenzao, Mudy Muswadiku, wameruhusiwa kuendelea kujisomea wakiwa gerezani ili kujiandaa na mtihani wa kidato cha nne unaotarajiwa kuanza Novemba 4.

Ruhusa hiyo imetolewa na mahakama baada ya Majaliwa Abdu, mwalimu ambaye ni miongoni mwa watuhumiwa katika shtaka hilo, kuwasilisha maombi matatu kwa mahakama jana, kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya pili katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

Majaliwa aliiomba mahakama kuwapatia hati ya mashtaka, pia wanaomba upelelezi wa kesi hiyo uwahishwe ili kama wanafunzi hawatakuwa na hatia waweze kurudi shuleni kuendelea na masomo na kujiandaa na mitihani inayowakabili baadhi yao.

Ombi la tatu, Majaliwa aliiomba mahakama kuwaruhusu wanafunzi wa kidato cha nne wanaotuhumiwa katika kesi hiyo kuruhusiwa kuwa na madaftari gerezani ili waweze kuendelea kujisomea na kujiandaa na mitihani inayotarajiwa kuanza Novemba 4.

Kutokana na maombi hayo, Wakili wa Serikali Haruna Shomari, alisema watuhumiwa hao watapatiwa hati hiyo ya mashtaka na pia vitu kama madaftari, vitabu na kalamu wanaruhusiwa kuwa navyo gerezani.

Aliwataka wanafunzi hao wawasiliane na mamlaka ya magereza waweze kuletewa madaftari, vitabu na kalamu waendelee kujisomea wakiwa gerezani kujiandaa na mitihani hiyo.

Katika kesi hiyo ya mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo aliyekuwa anasoma kidato cha nne, pia idadi ya watuhumiwa imeongezeka baada ya wanafunzi wengine wawili kuongezwa.

Wanafunzi waliongezwa ni Sharifu Amri (19) na Fahadi Abdulaziz Kamaga (20) na kusababisha idadi ya watuhumiwa kufikia wanafunzi sita, mwalimu mmoja na mlinzi mmoja wa shule hiyo.

Kesi hiyo ya mauaji namba 18/2019 inayosikilizwa na Hakimu Frola Kaijage, imetajwa kwa mara ya pili jana.

Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni wanafunzi Sharifu Huled (19), Abdalah Juma (19), Hussein Mussa (20) na mwingine ambaye jina lake linahifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Wengine ni mwalimu Majaliwa Abud (35) na mlinzi Badru Issa Tibagililwa (27).

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 30 itakapotajwa tena kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles