THERESIA GASPER – DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema hawezi kuumizwa kichwa na Zesco kwani anawafahamu vizuri mno, huku akidai kuongezewa nondo na kocha wa TP Mazembe ya DR Congo juu ya Wazambia hao.
Yanga inakabiliwa na mchezo raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco, unaotarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Timu hiyo ilitinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kuitoa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1 katika hatua ya awali.
Akizungumza baada ya mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jana, Zahera alisema wamejiandaa kuikabili timu hiyo na kupata ushindi nyumbani.
“Nafahamu timu ya Zesco ni kubwa na imecheza michuano hii mara nyingi lakini hata hivyo, kocha wa TP Mazembe (Bihayo Kazembe) alinipa mbinu zao kwa sababu alishacheza nao, hivyo hainipi ugumu kukabiliana nao,” alisema.
Alisema wachezaji wake wapo fiti isipokuwa Paul Godfrey ‘Boxer’ na Issa Bigirimana ambao ni majeruhi lakini wengine wanaendelea na programu ya mazoezi kama kawaida.
Zahera alisema mipango yao ni kushinda mchezo huo nyumbani kabla ya kwenda ugenini ili wajiwekee nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Alisema katika nafasi ya Boxer, anaweza akamchezesha Mapinduzi Balama ambaye alianza kumfanyisha mazoezi hayo jana huku akipanga kuendelea na leo.