33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Diwani kachero mkuu mpya

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amemteua Kamishna Diwani Athumani kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Dk. Modestus Kipilimba.

Siri ya kuwa Diwani alikuwa mtumishi wa TISS kwa mara ya kwanza ilifichuliwa na Rais Dk. John Magufuli Machi, 28 mwaka huu wakati akimwapisha Valentino Mlowola kuwa balozi mpya wa Tanzania nchini Cuba kazi iliyoambatana na kupokea taarifa ya utendaji kazi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Akizungumza baada ya kumwapisha Balozi Mlowola, Rais Magufuli alisema; “nilikuweka wewe kamishna wa polisi kuwa Mkurugenzi wa Takukuru kwa sababu unaweza kumshika mtu wakati wowote, ukishindwa kutumia sheria za Takukuru tumia za polisi.

“Huyu pia (Diwani) ni mtumishi wa TISS, kwahiyo hata kama mtumishi wa TISS amefanya kosa la rushwa unamshika.”

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, uteuzi wa mkurugenzi huyo mpya umeanza rasmi jana.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa Dk. Kipilimba atapangiwa kazi nyingine.

Akizungumza jana Ikulu Dar es Salaam baada ya kumwapisha Kamishna Diwani, Rais Magufuli alimtaka kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuweka mbele masilahi ya taifa.

Kabla ya uteuzi huo, Kamishna Diwani alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.

Mei mwaka 2015, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alimteua Kamishna Diwani kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Alishika nafasi hiyo hadi Oktoba 29 mwaka 2016, Rais Magufuli alipotengua uteuzi wake na kusema kuwa atapangiwa kazi nyingine.

Novemba 2016, ikiwa ni siku 24 tangu amtengue kwenye nafasi ya DCI, Rais Magufuli alimteua Diwani kuwa Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa wa Kagera.

Kabla ya hapo, mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mbeya.

Pia kabla hajawa RPC, aliwahi kushika nafasi nyingine za kiutendaji na kiutawala kama mlinzi wa IGP mstaafu Omari Mahita.

Pia alipata kuwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga.

Kwa upande wa Dk. Kipilimba, aliteuliwa kushika nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Idara ya Usalama Taifa Agosti 25 mwaka 2016, nafasi ambayo wakati huo iliachwa wazi na Rashid Othuman ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Kipilimba alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), nafasi iliyokuwa wazi baada ya aliyekuwa mkurugenzi wake, Dickson Maimu kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Vilevile aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Udhibiti (Director of Risk Management) wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kabla ya kupelekwa NIDA, Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Daftari na Tehama wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alijiunga BoT mwaka 1995 akiwa kama ofisa katika Idara ya Mambo ya Teknolojia ya Mawasiliano huku mmoja wa mabosi wake akiwa ni aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.

Kwa miaka kadhaa tangu utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mkurugenzi wa kwanza aliyeongoza idara hiyo nyeti alikuwa marehemu Emilio Mzena.

Wengine ni marehemu Dk. Laurence Gama, Mzee Hans Kitine ambaye alipoondoka nafasi hiyo ilishikiliwa na Dk. Augustine Mahiga ambaye kwa sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria.

Pia wengine ni pamoja na marehemu Luteni Jenerali Imrani Kombe na baadaye Apson Mwang’onda ambaye wakati wa uongozi wake aliiboresha idara hiyo na kuhakikisha muswada wa kuundwa kwa Idara ya Usalama wa Taifa kisheria unapelekwa bungeni na hatimaye ukasainiwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Baada ya Mwang’onda kustaafu Agosti 21 mwaka 2006 kwa mujibu wa sheria, nafasi hiyo ikashikiliwa na Rashid Othuman baada ya kuteuliwa na Rais wa awamu ya mne, Kikwete.

Othuman yeye alihudumu nafasi hiyo kwa muda wa miaka 10 tangu mwaka 2006 na baadaye Agosti 19 mwaka 2016, akastaafu na nafasi yake ikakaimiwa Mkurugenzi wa Mambo ya Ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa, George Madafa kabla ya Dk. Kipilimba kuteuliwa na Rais Magufuli.

Othuman anatajwa kuwa ni mtu aliyefahamika kuimarisha ulinzi pamoja na kuwa na maofisa wenye kuzingatia maadili ya kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles