AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
MAJERUHI watatu wa ajali ya lori la mafuta iliyotokea Msamvu mkoani Morogoro, waliokuwa wakipatiwa matibabu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wameruhusiwa jana baada ya afya zao kuimarika, huku wakishauri watu kutosogelea lori la mafuta likipata ajali.
Walioruhusiwa jana ni kati ya 11 waliokuwa wakipatiwa matibabu hospitalini hapo miongoni mwa 47 waliofikishwa Agosti 11 baada ya ajali kutokea Agosti 10.
Wengine 36 walifariki dunia wakiwa wanaendelea na matibabu hospitalini hapo na kufanya vifo vilivyosababishwa na ajali hiyo kuwa 104.
Akitoa taarifa ya kuruhusiwa majeruhi hao jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma MNH, Aminiel Aligaeshi, alisema majeruhi hao wanaruhusiwa wakaendelee na maisha yao huku wakihudhuria kliniki.
“Hivi tunavyoongea majeruhi 10 wapo katika wodi za kawaida na mmoja yupo ICU (Chumba cha Uangalizi Maalumu), lakini hapumui kwa mashine.
“Hapa tumekuja na majeruhi wawili, wengine wako wodini, mpaka jioni tutaangalia ni yupi anayefaa kuruhusiwa kwani wako wawili.
“Tunamshukuru Rais kwa kuhakikisha kuwa majeruhi wanahudumiwa, pia wananchi ambao walikuwa wakitoa misaada, damu na pia kuwaombea kwa vikundi, makampuni, mtu mmoja mmoja, tunawashukuru wote,” alisema Aligaeshi.
DAKTARI AELEZA JITIHADA WALIZOFANYA
Daktari Bingwa wa Upasuaji MNH, Edwin Mrema, alisema majeruhi wa moto wanatibiwa na idara mbalimbali na kwa hatua tofauti tofauti.
“Matibabu ya madhara ya moto si ya mtu mmoja, ni timu ya zaidi idara sita, mfano kuna wataalamu wa saikolojia, upasuaji, huduma za viungo na idara nyingine,” alisema Dk. Mrema.
Alisema majeruhi 11 waliobaki wanaendelea vizuri kutokana na kuendelea kupona sehemu ya miili yao, ikiwemo mfumo wa hewa na vidonda.
“Hawa majeruhi tuliwapokea wakiwa katika hali ya hatari na sasa sehemu kubwa ya vidonda vimeshapona, pia mfumo wa hewa na upumuaji umekuwa mzuri, kiujumla wanaonekana kuimarika kiafya.
“Matibabu ya majeraha ya moto ni ya muda mrefu, hivyo hata wagonjwa walioruhusiwa wataendelea na kliniki ya nje kwa siku watakazopangiwa ili kama kuna kitu cha kuwasaidia tuwasaidie.
“Pia watahudhuria kliniki ya kisaikolojia kwa sababu wanapopata majeraha kama haya wanaathirika kisaikolojia, tukumbuke pia hawa ni watu waliotoka kwenye jamii, wana familia, kazi, hivyo wanahitaji huduma za kisaikolojia ili wakirudi huko waweze kukabiliana na mazingira,” alieleza Dk. Mrema.
Alisema majeruhi hao pia watapata huduma ya viungo kwani ingawa kwenye ngozi vidonda vimeisha, bado wanaweza kupata makovu baada ya miezi miwili au mitatu.
“Walio wodini tayari walishaanza kufanya mazoezi ya viungo na bado wataendelea kupata wakati watakapokuwa wanakuja kliniki,” alisema.
Dk. Mrema alisema majeruhi mmoja kati ya 11 waliobaki alifanyiwa upasuaji wa kuondolewa miguu kutokana na kuungua na mwingine alifanyiwa upasuaji baada ya mfumo wa chakula kushindwa kufanya kazi vizuri.
“Kuna wagonjwa wawili walipata ‘complication’ kubwa, ilifanya tuwapeleke chumba cha upasuaji ambao mmoja aliungua miguu, huyo ilibidi madaktari wamtoe viungo kwani vikiendelea kubaki ataathirika zaidi na anaendelea vizuri.
“Mwingine alipoteza chumvi chumvi, hali hiyo ikawa inamletea shida kuzirudisha kwenye usawa unaotakiwa, mfumo wake wa chakula ukashindwa kufanya kazi vizuri akashindwa kujisaidia, tulimfanyia upasuaji na sasa anaendelea vizuri,” alibainisha Dk. Mrema.
Alisema kuwa matibabu ya majeraha ya moto yanachukua muda mrefu hivyo hata walioruhusiwa bado wataendelea na matibabu.
MAJERUHI WATOA USHAURI
Majeruhi waliotoka hospitali jana walitoa shukrani kwa watu mbalimbali akiwamo Rais Dk. John Magufuli kutokana na msaada na mchango mkubwa alioutoa katika kurejesha afya zao.
Mmoja wa majeruhi hao, Mikidadi Issa alisema kuwa ingawa amepona, lakini kutokana na ajali hiyo amepoteza ndugu wengi.
“Kwanza namshukuru Mungu kwa kunirejeshea tena afya yangu, namshukuru Rais wetu alitusaidia sana, alinipa Sh 500,000 wakati naumwa, lakini pia nawashukuru Watanzania wote waliotoa misaada yao na wengine waliotuombea,” alisema Mikidadi.
Majeruhi mwingine, Shaban Omary aliwashauri watu pindi ajali itakapotokea wasijihusishe kuchukua vitu bali wajitahidi kuwa mbali, hasa ajali ya lori la mafuta.
“Mimi nilikuwa machinga, lakini sasa nikirudi naenda kuwa mkulima, naamini nitakuwa na maisha mazuri, lakini nawashauri watu pindi ajali ya lori la mafuta itakapotokea wasijaribu kusogelea kwa sabubu sasa tumepoteza watu wengi na wengi ni vilema,” alishauri Omary.