Ujerumani kuipa Tanzania Sh bilioni 26 kuboresha afya

0
486

Mwandishi wetu – Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainabu Chaula, kwa niaba ya Serikali amesaini mkataba wa makubaliano wa Sh  bilioni 26.6 wa miaka mitatu na Serikali ya Ujerumani kuimarisha afya ya msingi nchini.

Akizungumza jana, Dk. Chaula alisema kwa mwaka huu wameweka makubaliano ili fedha hizo zitolewe kwa wakati mmoja na kuweza kutumia mfumo wa ‘Force Account’ kama walivyoweza kutumia kwenye ujenzi wa vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa katika kuboresha sekta ya afya nchini.

 “Tumeanza mahusiano tangu mwaka 1961, kuanzia  mwaka 2003 huu ni mkataba wa tano, na mkataba wao ni wa miaka mitatu mitatu ambao umejikita katika kuimarisha afya ya msingi katika halmashauri zetu katika vituo vya afya pamoja na zahanati,” alisema.

Dk. Chaula alitaja maeneo yatakayonufaika na mkataba huo ni uhimarishaji wa taarifa, afya ya mama na mtoto, uzazi wa mpango, bima ya afya kwa wajawazito pamoja na utawala bora, jinsi ya kutumia fedha hizi kulingana na kanuni na taratibu za nchi.

“Huu ni mwendelezo wa mkataba wa miradi mingi ambayo tumeifanya katika kuboresha sekta ya afya, kama mnavyokumbuka hadi sasa hivi tumeshafanyia ukarabati vituo vingi vya afya.

“Tuna vituo 470 ambavyo vimeshafanyiwa ukarabati  tangu mwaka 2017 katika ngazi za zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya,” alisema.

Aidha, Dk. Chaula alisema Serikali iliwekeza shilingi

bilioni mia moja na milioni mia tano katika hospitali za halmashauri.

 “Zamani hawa wenzetu walikuwa wakitumia wakandarasi wao na pesa wanakaa nazo, hivyo tumekaa nao na kukubaliana kama fedha hizi watazitoa kwa wakati mmoja ili tuweze kuzisimamia kama tulivyofanya kwenye vituo tulivyoanza ili kuweza kutekeleza kwa umakini na kupata matokeo makubwa katika kipindi hiki,” alisema Dk. Chaula. 

Kwa upande wa hali ya uzazi, mama na mtoto, alisema hivi sasa inakaribia asilimia 80 ya kina mama wajawazito wanajifungulia vituo vya afya tofauti na zamani ambapo kulikuwa na changamoto kubwa kwani wengi walikuwa wanajifungulia majumbani kwa asilimia 39 na kufuatia na asilimia 59.

“Hii ni kutokana na kuboreshwa kwa vituo vya afya pamoja na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kina mama wote wanajifungulia vituo vya afya,” alisema Dk. Chaula.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here