MANCHESTER, ENGLAND
KIUNGO wa Manchester United, Paul Pogba, ameweka wazi vitendo vya kibaguzi anavyofanyiwa kwenye mitandao ya kijamii vinamfanya azidi kukomaa katika soka.
Mchezaji huyo ambaye amepanga kutaka kuondoka katika kipindi hiki cha kiangazi, wiki moja iliopita ilikuwa ngumu kwake baada ya kukosa mkwaju wa penalti katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Wolves ambapo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mbali na kushindwa kuisaidia timu, lakini wachezaji wenzake pamoja na baadhi ya mashabiki walionekana kumkingia kifua huku wakiamini mtu yeyote anaweza kukosa penalti, ila wengine walionekana kumtupia lawama kwa kuonesha wazi vitendo vya kibaguzi.
“Wazazi wangu walipambana kwa ajili ya kizazi changu kije kuwa huru leo, niweza kuwa huru kutembea popote, nicheze mpira kwa uhuru. Masuala ya ubaguzi hayana maana yoyote, lakini kwa kunifanyia hivyo ninaamini kunanijenga na kunanifanya nipambane kwa ajili ya kizazi kijacho,” alisema mchezaji huyo.
Kitendo hicho cha kibaguzi ambacho amefanyiwa mchezo huyo kiliwaamsha wachezaji mbalimbali wa timu hiyo kama vile Marcus Rashford, David de Gea na Harry Maguire.
Kwa upande wa Maguire alitoa ushauri kwa wamiliki wa mitandao kuwafanya watu wajisajili kwa kutumia pasi ya kusafiria ili kuweza kupunguza masuala kama hayo ya kibaguzi kwa kuwa watakamatwa kwa urahisi.
“Mitandao ya kijamii inatakiwa kubadilika, vizuri kwa watu wanaojisajili kuitumia wakasajiliwa kwa kutumia pasi zao za kusafiria au leseni ili waweze kujulikana kwa urahisi. Ubaguzi unatakiwa ufikie mwisho kwa kupitia mtandao wa Twitter na Instagram,” alisema Maguire.
“Manchester United ni familia, Paul Pogba ni sehemu ya familia hiyo, ukimshambulia kwa kumbagua sawa na kuwabagua au kuwashambulia Manchester United wote,” alisema Rashford.
Manchester United wenyewe wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii na kupinga vikali kitendo hicho cha ubaguzi kilichooneshwa na mashabiki wake wiki iliopita na wamemtaka mchezaji huyo kuwa na amani.