PETER FABIAN, RORYA
VIONGOZI na wananchi wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, wanamshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kuwajengea hospitali ya wilaya ambao ujenzi wake utagharimu Sh bilioni 1.5 hadi kukamilika.
Kukamilika kwa hospitali hiyo kutawasaidia wananchi kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika wilaya za Tarime, Musoma na nchi jirani ya Kenya.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa Kijiji cha Ingiri Juu, Mkuu wa Wilaya hiyo, Saimon Chacha alisema kukamilika ujenzi huo kutaondoa changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu wilaya za jirani zaidi ya kilomita 60 na hadi 80 kwenda nchi jirani ya Kenya kama ilivyo sasa.
” Tunamshukuru Rais Dk.John Magufuli kwa kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Wilaya ya Rorya kutujengea hospitali ambayo itaondoa adha ya kutembea umbari mrefu kutafuta huduma za afya hali iliyosababisha baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha,” alisema.
Alisema ushirikishwaji wa wananchi umesaidia ujenzi wa hospitali kwenda kasi hadi kufikia hatua ya ukamilishaji wa majengo saba yaliyopo, ikiwa na hatua ya kupakwa rangi, kuwekwa vigae, milango, dali, madirisha na kukamilisha mifumo ya maji na umeme ambapo mafundi wanaendelea kukamilisha uliofikia zaidi ya asilimia 80, licha ya kuwepo changamoto ya fedha za ujenzi.
Kwa upande wa wananchi, Avelin Silvely, alimpongeza rai kusikkiliiza kero za wananchi wanyonge na kuzitekeleza kwa vitendo.
Mkazi wa Kijiji cha Utegi, Noelina Daniel alisema kukamilika ujenzi huo kutakuwa ukombozi sekta ya afya kutoa huduma walizikosa muda mrefu.
Naye Mbunge wa Rorya, Lameck Airo (CCM) alisema wamepita viongozi wengi ambao hawakujenga hospitali ya wilaya, lakini Rais Magufuli alipoingia alitoa Sh bilioni 1.5 za ujenzi huo.
“Rais Dk. Magufuli ni kiongozi mchapa kazi na mfano wa kuigwa anayesikiliza wanyonge, aliposikia kilio chetu Rorya licha ya kutofika na kufanya ziara, akatoa fedha za ujenzi,”alisema.
Aliwataka wanaanchi kumuunga mkono kujiiletea maendeleo kwa kuweka kando tofauti zao za itikadi za kisiasa.