26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Wakimbizi 2000 kurudishwa Burundi

Editha Karlo, Kigoma

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametangaza kuwarudisha nchini Burundi wakimbizi wote kuanzia Oktoba mosi, mwaka huu.

Baada ya wakimbizi wote kurudishwa makwao, makambi waliyokuwa wanatumia yatafugwa rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari  mkoani Kigoma jana Waziri Lugora alisema huo ni msimamo wa Serikali ya Tanzania.

Alisema kuanzia sasa ni wakimbizi wote wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye makambi mbalimbali mkoani Kigoma wanaondoka katika kipindi kifupi kijacho na hakuna tena mjadala kuhusiana na jambo hilo.

Alisema katika hilo watatekeleza makubaliano ya  pande hizo tatu ambazo ni Serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR)  kurudisha wakimbizi 2,000 kila wiki kwenda Burundi.

Alisema Tanzania na Burundi zimekubaliana kusimamia kazi hiyo hata kama hakutakuwapo  msaada wowote kutoka jumuia za kimataifa kusaidia kurudishwa kwao kwa wakimbizi hao.

 Alisema sababu kubwa iliyowafanya  wakimbizi kukimbia nchi yao, ni  kuwapo hali mbaya ya usalama ,lakini sasa hali haipo na wakimbizi hao wanapaswa kurejea.

Alisema Serikali ya Tanzania inatekeleza mikataba ya kimataifa kuhusu kuwapokea, kuwahifadhi na kuwarudisha kwao wakimbizi na haitawalazimisha wakimbizi kurudi kwao, lakini wakati wanaingia nchini sababu  ilikuwa kutokuwapo amani.

“Amani imerejea Burundi,sababu hii haitoi nafasi kwa wakimbizi  kupata hadhi ya ukimbizi nchini, hilo ni agizo la Serikali,”alisema.

Aliwaonya baadhi ya watu na taasisi  zinazotoa huduma kwa wakimbizi  kuzorotesha kazi ya kuwaondoa kwa sababu  ya kuwarubuni, kupotosha namna Tanzania na Burundi zinavyosimamia.

Alisema taasisi hizo, hutoa kauli za kuwatia woga wakimbizi  kwamba Burundi hakuna amani ili wasirudi kwao.

“Yeyote atakayebainika kuhusika na hilo ikiwemo mtu binafsi, mashirika atashughulikiwa ipasavyo,”alisema.

 Akitoa takwimu kuhusu hali hiyo, alisema kazi ya kuwarudisha wakimbizi wa Burundi lilianza mwaka 2017 na hadi sasa  74,439 wamerejea, hakuna taarifa zozote wakimbizi hao kuugua au wana hali mbaya ya kiusalama.

Kwa nyakati tofauti, akizungumza kwenye mikutano ya hadhara na wakimbizi kwenye kambi Nduta na Mtendeli,  Waziri wa Mambo ya Ndani na Maendeleo Vijijini wa Burundi, Pascal Barandagiye alisema  hakuna sababu yeyote ya raia wake kuendelea kuwa wakimbizi kwa sababu hali ya utulivu ipo nchini mwaoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles