Theresia Gasper -Dar es salaam
KIKOSI cha JKT Tanzania kimeanza mazoezi rasmi ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba, unaotarajiwa kuchezwa Agosti 29, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hiyo ilijichimbia Zanzibar kwa kambi ya wiki tatu, kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya , kabla ya kurejea Dar es Salaam yaliko makao yake makuu Jumatatu wiki hii, ambapo wachezaji walipewa mapumziko ya siku nne ksiha jana kuingia kambini.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdallah Mohammed ‘Bares’, alisema wameanza kuipigia hesabu Simba, kwa kuangalia mechi zao ili kutafuta mbinu za kuikabili na kupata ushindi.
“Tumeanza kambi leo (jana), baada ya mapumziko mafupi, tunafanya mazoezi asubuhi kujiandaa na mchezo wetu wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Simba,” alisema.
Alisema kwa kuzingatia maandalizi wanayofanya, anaamini watauanza msimu mpya vizuri tofauti na ule uliopita.
“Lengo letu ni kuanza msimu kwa kuvuna pointi tatu, tumefanya mandalizi ya kutosha, tulikuwa Zanzibar kule tulipata wasaa mzuri wa kujiandaa.
“Kipindi hiki kifupi kilichobakia niendelea kutafutia ufumbuzi wa kasoro nilizoziona katika michezo yetu ya kirafiki kabla ya kukabiliana na Simba, naamini tutafanya vizuri,”alisema Bares.