*Vikao vinne vya Halmashauri Kuu vyawaweka kikaangoni Katibu Mkuu, manaibu wake, tume yaundwa
*Maaskofu wagawanyika, wengine wamtaka Shoo baadhi Munga, hoja za migogoro, ubadhirifu zaibuka.
Waandishi wetu-ARUSHA
WAKATI maelfu ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wakielekeza masikio yao Arusha, ambako leo maaskofu na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 20 kutoka pande zote nchini wanapiga kura kumchagua Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo, uchaguzi huo unatajwa kuwa si mwepesi.
Mazingira ya ndani na nje ya vikao vinne vya Halmashauri Kuu ambavyo vimekwishafanyika hadi sasa Chuo Kikuu cha Makumira cha kanisa hilo kilichopo mkoani hapa, yanaonyesha atakayepita kuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo, itakuwa imefanyika kazi kubwa na ya ziada.
Taarifa zilizolifikia MTANZANIA kutoka Arusha yaliko makao makuu ya kanisa hilo, zinaeleza kuwa kikao cha uteuzi wa majina kitafanyika leo asubuhi baada ya kushindikana jana jioni kutokana na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Frederick Shoo kuhudhuria msiba wa mama mkwe wake.
Askofu Dk. Shoo ambaye jina lake litajumuishwa katika orodha ya majina ya maaskofu watakaoingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho, anaonekana kulazimika kuhitaji sapoti kubwa atakapopambana na majina mapya kama Askofu Stephen Munga ambaye ni Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.
Kuanza kutajwa kwa jina la Askofu Munga ambaye anaonekana kuungwa mkono na maaskofu wengi tofauti na Dk. Shoo ambaye anaonekana kuhitaji msaada wa walei, ndiko kunaelezwa kuufanya uchaguzi huu kuwa mgumu zaidi.
Kuvuja kwa taarifa hizi mpya, kumekuja wakati ambao baadhi ya vyombo vya habari vimekariri wajumbe wakiwataja kwenye orodha hiyo maaskofu wengine kama wa Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk. Abednego Keshomshahara na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa.
Dhana kwamba uchaguzi huu si mwepesi hasa kwa upande wa Dk. Shoo, inapewa nguvu na taarifa mpya zilizotufikia, ambazo zinadai kuwa vikao vya Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo vya siku nne pamoja na mambo mengine viligubikwa na majadiliano makali kuhusu migogoro isiyokwisha kwenye baadhi ya dayosisi zake kama Tanganyika na Kusini unayohusisha sharika za Sumbawanga, Mpanda, Mtwara, Mafinga, Makete na Mufindi.
Hoja nyingine ni ubadhirifu wa fedha na mali za kanisa, likiwamo suala la kufungwa kwa Chuo Kikuu cha Makumira cha mkoani Mbeya kutokana na masuala ya fedha hali inayotajwa kutishia chuo hicho kupokwa.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinadai kutokana na hayo na mengine, vikao vya Halmashauri Kuu vimefikia uamuzi wa kumwondoa Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Brighton Kilewa na manaibu katibu wakuu wote.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, tume maalumu imeteuliwa ili kumpata Katibu Mkuu mpya atakayefanya kazi ya kuunda upya uongozi ulio chini yake kwa maana ya sekretarieti pamoja na wakuu wa vitengo.
Kwa siku zote nne timu ya MTANZANIA ambayo imepiga kambi jijini Arusha, imeshuhudia ulinzi mkali ikiwa ni pamoja na wanahabari kutokuruhusiwa kuingia eneo la mkutano zaidi ya wanahabari wa vyombo vinavyomilikiwa na kanisa hilo.
Katibu wa Idara ya Mawasiliano Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Mathayo Saruma, alipotafutwa kuzungumzia uchaguzi huo, alisema hakuna lililoendelea kuhusu uchaguzi bali zilikuwa ni shughuli nyingine.
Alisema leo ndiyo suala la uchaguzi litashughulikiwa na kama kutakuwa na majina zaidi ya Dk. Shoo yatajulikana.
“Mkutano wa leo (jana) ulikuwa na ajenda mbili ambayo ni uchumi kwa misingi ya kanisa na ujenzi wa familia imara. Kuhusu uchaguzi hakuna lililoendelea, wagombea na mengine tutajua kesho (leo),” alisema.
Taarifa iliyotolewa na Mchungaji Saruma jana ilieleza kuwa Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani, Askofu Mkuu Dk. Panti Filibus Musa kutoka Kanisa la Kilutheri Kristo Nigeria, akiendelea kufundisha somo kuu, ametaja tabia kuu tatu za uchungaji.
“Siyo jambo la kulazimishwa, bali ni wito na anapaswa kufanya kwa furaha, asiwe kama maksai ambao bila kiboko hawalimi, ninajua kuna ambao wamekuwa viongozi wa kanisa kwa kulazimishwa na familia, heshima, au kujaza nafasi, lakini inapasa kuelewa uchungaji ni wito.
“Pili si kwa ajili ya faida binafsi au sababu zisizo sawa kama vile madaraka au pesa, hata hivyo si vibaya kwa wale wanaohudumu kupata ujira, bali kuwa kiongozi wa kanisa sababu isiwe kupata faida binafsi.
“Leo injili imekuwa biashara na tunaonywa kuwa kupenda fedha kusiwe sababu ya utauwa, tunajua kuwa ulafi umezua migogoro ndani ya kanisa, Paulo ni kielelezo cha jinsi alivyotunza mahitaji yake na ya wale aliohudumu pamoja naye. Alikataa kula bila kulipia. Na ukiwa mtumishi ukitembelea watu, japo hawajala kuku miezi mingi, lakini kwa kuwa mchungaji anakuja watamwandalia kuku,” alisema.
Alisema wachungaji hawapaswi kutumia ukarimu wa watu kuwanyonya na kuwakandamiza ili kujitajirisha.
Askofu Dk. Musa alisema huko Nigeria ni rahisi kusikia kiongozi wa kanisa kusema roho ameniambia mmoja wenu atanipa ufunguo wa gari lake hapa, semeni amen.
ASKOFU DK. SHOO
Dk. Shoo ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alichaguliwa Agosti 2015 baada ya kuwashinda maaskofu wenzake wawili.
Maaskofu waliochuana na Dk. Shoo kuwania nafasi hiyo baada ya kupendekezwa na Halmashauri Kuu ya KKKT, ni Askofu Dk. Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Askofu Charles Mjema wa Dayosisi ya Pare.
Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Dk. Malasusa, alimtangaza Dk. Shoo kuwa mkuu wa kanisa hilo kwa kipindi cha miaka minne baada ya kupata kura 153, huku Dk. Munga akipata kura 67, ikiwa ni baada ya uchaguzi huo kurudiwa mara tatu kutokana na mshindi kutopata zaidi ya theluthi mbili ya kura zote.
Kanuni za uchaguzi za KKKT zinaeleza kuwa mshindi atapatikana kwa kupata kura zisizopungua theluthi mbili ya zote zilizopigwa na iwapo mshindi hatapatikana katika duru la kwanza, majina mawili yaliyopata kura nyingi ndiyo yatakayopigiwa tena kura.
Iwapo theluthi mbili haitapatikana katika duru la pili, kura ya wingi au uchache itatumika kwa duru la tatu ili kumpata mshindi.
Katika kuhakikisha mshindi anapatikana, mkutano huo ulilazimika kutumia hatua ya wingi wa kura na Dk. Shoo kuibuka mshindi.
Katika awamu ya kwanza, Askofu Mjema alipata kura 53, Dk. Munga 81 na Dk. Shoo kura 86, idadi ambayo haikufika theluthi mbili ya kura zote kulingana na kanuni za kanisa hilo jambo lililosababisha uchaguzi kurudiwa mara ya pili.
Dk. Malasusa alitangaza matokeo ya awamu ya pili ya kura zilizopigwa ambapo Askofu Munga alipata 94 na Dk. Shoo 124. Kura moja ikiharibika.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wajumbe wa Halmashauri Kuu walipitisha majina hayo matatu ya maaskofu waliowania nafasi hiyo na kuyapeleka kwenye mkutano huo ili yapigiwe kura.
Wajumbe hao mara baada ya kupewa karatasi za kupigia kura, walikwenda katika vyumba maalumu kumchagua askofu wanayemtaka, na baada ya kuchagua walitakiwa kurejea ukumbini na kutumbukiza karatasi hizo katika vifaa vilivyoandaliwa kuhifadhia kura hizo.
MAASKOFU KKKT
Kanisa hilo lina maaskofu 26 ambao ni pamoja na Dk. Shoo ambaye ndiye mkuu wa kanisa hilo kwa sasa.
Wengine na dayosisi zao kwenye mabano ni Benson Bagonza (Karagwe), Stephen Munga (Kaskazini Mashariki), Alex Mkumbo (Kati), Blaston Gaville (Iringa), Abednego Keshomshara (Kaskazini Magharibi), Andrew Gulle (Mashariki Ziwa Victoria), Emanuel Makala (Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria) na Chediel Sendoro (Mwanga).
Pia wapo Charles Mjema (Pare), Elias Nassari (Meru), Solomon Massangwa (Kaskazini Kati), Jacob Ole Paulo (Morogoro), Michael Adam (Mkoani Mara), Isaya Mengele (Kusini Njombe), Job Mbwilo (Kusini Magharibi), Renard Mtenji (Ulanga Kilombero) na Ambele Mwaipopo (Ziwa Tanganyika).
Maaskofu wengine ni Alex Malasusa (Mashariki na Pwani), Edward Mwaikali (Konde), Wilson Sanga (Kusini Kati) Amon Mwenda (Ruvuma), Lucas Mbedule (Kusini Mashariki), Amon Kinyunyu (Dodoma), Nicolaus Nsanganzelu (Mbulu) na Isaack Kissiri Laiser (Magharibi Kati).