25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri, mabalozi wajipanga kutekeleza maazimio ya SADC

NORA DAMIAN Na ANDREW MSECHU – dar es salaam

BAADA ya kukamilika mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwamo mawaziri, mabalozi na makatibu wakuu, wameelezea namna watakavyosaidia utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa.

Mkutano huo ulihitimishwa juzi kwa kupitisha maazimio zaidi ya 30 yanayotakiwa kutekelezwa kwa mwaka mmoja chini ya uenyekiti wa Rais Dk. John Magufuli.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, Dar es Salaam juzi, viongozi hao walisema watahuisha sehemu ya maazimio hayo katika sera na mipango ya taasisi wanazosimamia, kuhakikisha uenyekiti wa Tanzania katika jumuiya hiyo unakuwa na mafanikio.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema mkakati wao ni kuendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kujenga viwanda ili Tanzania iwe ni nchi rahisi kufanya biashara.

“Tuutumie huu mwaka vizuri katika kipindi ambacho Rais wetu ni mwenyekiti, anataka kuona ile ‘theme’ ya SADC inatekelezwa kwa vitendo, yaani tunajikita kwenye uchumi wa viwanda ili kutengeneza ajira kwa wingi.

“Kikubwa Watanzania tuchape kazi kama ni mkulima ongeza bidii ili mavuno ya msimu unaokuja yawe makubwa kuliko sasa, tupate malighafi za kutosha kupeleka kwenye viwanda,” alisema Bashungwa.

Alisema wanawasaidia wafanyabiashara na wenye viwanda kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa sababu wao wakifanikiwa hata mkakati wa Serikali wa kuongeza uwekezaji utafanikiwa na watakuwa mabalozi wa kuwaambia wengine waje kuwekeza Tanzania kwa sababu mazingira ni mazuri.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema watasimamia maazimio yote kuhakikisha biashara inakua kati ya nchi na nchi na kuongeza ajira kwa kutegemea uchumi wa viwanda.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema kutokana na mkazo mkubwa wa jumuiya hiyo kuelekezwa kwenye ujenzi wa viwanda, watahakikisha wanaongeza thamani ya mazao mbalimbali kutoa fursa za ajira na kuongeza mapato.

“Kuna haja ya nchi zilizoko Kusini mwa Afrika badala ya kuanza kuagiza bidhaa kutoka maeneo mbalimbali ni muhimu kuangalia kama zinapatikana ndani ya nchi wanachama ili tuweze kuuziana wenyewe kwa wenyewe.

 “Ni wakati mwafaka wa kuongeza thamani mazao yetu tutengeneze ajira kwa wingi na kuziwezesha nchi kuuziana na nyingine,” alisema Hasunga.

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk. Willbroad Slaa, alisema ni vyema Watanzania wakajifunza kutangaza mazuri yanayofanyika nchini ili kuwavutia watu wengi zaidi kuja kuwekeza.

“Mfano unapowashawishi wawekezaji kwamba kuna fursa nyingi twendeni Tanzania, unakuta wameshapewa taarifa kwamba Tanzania hapafai, kuna mauaji, kuna watu wanapotea na tungeachia hapo ingekuwa afadhali, wanasema ni Serikali imefanya hilo… kabla hujahukumu unapaswa kufanya utafiti wa kutosha,” alisema Dk. Slaa.

Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi, alisema licha ya nchi kupiga hatua kubwa za kimaendeleo, lakini watu wengi wamekuwa wakiaminishwa mambo mbalimbali yanayoendelea kwa mtazamo hasi na kuwavunja moyo.

“Niliambiwa Kariakoo biashara zimefungwa, lakini nimekuja nimekuta hata nafasi ya kufanya biashara hakuna, wakasema ndege hazijai, mimi nimekwenda kutaka tiketi nikaambiwa zimejaa wiki nzima,” alisema Masilingi.  

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante ole Gabriel, alisema watalitumia soko la SADC lenye watu milioni 327 kuuza bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo, yaani nyama, maziwa na ngozi.

“Kupata fursa ya kuwa mwenyekiti unatanua fursa za kibiashara na sisi katika mazao yetu ya mifugo tunaamini kwamba tutapata soko kutokana na idadi kubwa ya watu walioko SADC,” alisema Profesa Gabriel.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera, alisema mkoa huo unazalisha kwa wingi bidhaa mbalimbali, hivyo watakwenda kuongeza thamani za mazao ili wauze katika soko la SADC.

“Sisi mkoani kwetu tunazalisha bidhaa nyingi, mpunga zaidi ya tani 250,000, mahindi zaidi ya tani 800,000 na tuna ziada ya chakula tani 150,000, tutakwenda kujikita zaidi kwenye nchi za SADC kwa sababu nyingi zina changamoto ya chakula,” alisema Homera.

Alisema pia wamekuwa wakiuza bidhaa zao katika nchi za Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya tani 20,000 hadi 25,000 kwa msimu.

KATIBU MTENDAJI SADC

Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Dk. Stagomena Tax, alisema katika kipindi chake cha uongozi, hajawahi kuona mkutano uliofana kama wa mwaka huu uliofanyika nchini.

Alisema ni wazi mkutano huo, ni mwanzo mpya wa mafanikio na utatuzi wa changamoto zinazoikabili SADC ambayo imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanafikiwa.

“Katika mwaka huu, SADC inaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha kaulimbiu ya mkutano huu ambayo inalenga uwekezaji katika viwanda na uzalishaji wa ajira inafanikiwa. Hii inalenga katika uwekezaji kwenye teknolojia na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanafanikiwa.

“Hii itawezesha kuleta mabadiliko ya namna mpya ya kupambana na umasikini, kuinua viwango vya maendeleo katika kanda hii na Bara la Afrika kwa ujumla,” alisema.

Alisema ameshuhudia namna Wiki ya Viwanda ilivyofana na sekta binafsi ilivyochangamkia fursa kupitia wiki hiyo, ambayo kwa Tanzania imekuwa na upekee wa aina yake tofauti na alivyowahi kushuhudia katika nchi nyingine.

Alisema uwekezaji wa uhakika kwenye viwanda unahitaji ushirikiano baina ya sekta ya umma, sekta binafsi na washirika wengine wa maendeleo kikanda na kimataifa, na kwamba sekta binafsi ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya watu, kwa kuwa ndiyo inayotegemewa kuzalisha ajira, kuinua uchumi na kuchangia mapato ya Serikali na kuinua hali za maisha za watu.

Alisema ili kuwezesha sekta binafsi iwe kinara katika agenda ya viwanda, inahitaji kuwa na ushindani, kwenda na wakati na kuunganishwa kikamilifu kikanda na kimataifa.

Dk. Tax alisema katika kufikia malengo hayo kwa sekta binafsi, inahitajika uwepo wa taaluma stahiki, uwezo wa kiteknolojia, miundombinu inayowezesha uwekezaji kwenye viwanda na uwepo wa sera nzuri za kikanda na kitaifa kuwezesha sekta hiyo.

Alisema ushirikiano wa pande tatu wa kikanda unaohusisha jumuiya ya Comesa, EAC na SADC ulioanzishwa mwaka 2015 na Eneo Huru la Bara la Afrika (AfCFTA) ambayo makubaliano baina ya pande hizo yalitiwa saini Mei 30 mwaka huu, utasaidia ushindani na kuongeza fursa kwenye soko jipya lenye watu zaidi ya bilioni 1.2.

Dk. Tax alisema Tanzania sasa inawajibika pia kusimamia utekelezaji wa mpango wa uwekezaji kwenye viwanda wa 2015 – 2010, itifaki katika viwanda na  mkakati wa madini pamoja na mkakati wa utekelezaji kwa pamoja bado vinahitaji usimamizi imara kwa utekelezaji.

Alisema mpango wa madini kikanda una nia ya kuweka mazingira mazuri ya urutubishaji na uendelezaji wa rasilimali hiyo muhimu kikanda, kwa nia ya kuhakikisha rasilimali hiyo ambayo inapatikana kwa wingi katika ukanda wa SADC inatumiwa ipasavyo kwa maendeleo ya nchi na kanda nzima.

“Kwa kutambua mchango wa viwanda vidogo na vya kati (SMEs), sekretarieti kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa (UN) ya Uchumi kwa Afrika, imeandaa utaratibu wa kuangalia namna ya kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu na kuwa mshiriki mkuu katika uwekezaji wa viwanda,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amevipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa ya kiuzalendo na weledi wa hali ya juu katika kutangaza mkutano huo.

Dk. Mwakyembe alitoa pongezi hizo jana jijini Dodoma.

Alisema uandishi wa habari wa kujenga na kukosoa ambao una lengo la kurekebisha, unahitaji kupongezwa kwa kuwa unasaidia jamii na Serikali kuleta maendeleo ya haraka kwa taifa.

“Waandishi wa habari mbali na kuutangaza mkutano wa 39 wa SADC, wametumia taaluma yao kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini kupitia sekta mbalimbali, ikiwamo uwekezaji katika viwanda, utalii, uchukuzi na nyinginezo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles