27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Video ya kina mbowe yaonyeshwa mahakamani

Kulwa Mzee -Dar es salaam

VIDEO inayodaiwa kuonyesha viongozi wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe wakiandamana, imeonyeshwa mahakamani.

Katika video hiyo, hakuna mshtakiwa aliyeonekana kuwa miongoni mwa waandamanaji.

Wabunge mbalimbali wa chamama hicho walihutubia jukwaani, lakini Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, hakuonekana wakati wabunge wengine wakisalimia wananchi.

Video hiyo ilionyeshwa jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Koplo Charles ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi. aliweka ‘tape’ ya kwanza ambayo ilionyesha wabunge mbalimbali wakihutubia wakiwemo, aliyekuwa Mbunge wa  Ukonga Mwita Waitara, Mbunge Ubungo, Saed Kubenea, Peter Lijualikali (Kilombero), David Silinde (Mbozi Magharibi) na aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye.

Wengine ambao ni washtakiwa katika kesi hiyo walioonekana ni Mbowe, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko hakuonekana katika video hiyo.

YALIYOSIKIKA KATIKA VIDEO

Katika video hiyo, Waitara ambaye sasa ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, alisikika akiwataka polisi watulie kama maji ya mtungi.

Heche alidai Serikali ya Magufuli watu wanauawa, wanapotea, kazi kwao wananchi kurudisha amani ya nchi.

Msigwa pamoja na mambo mengine, alisikika akisema kubeba panga, kisu, rungu, shoka, jiwe hakuhitaji kuomba kibali cha polisi.

Bulaya alisikika akisema hawana historia ya kuibiwa, yuko na kikosi chake, polisi watawalinda na aliwaomba wananchi wampigie kura Salum Mwalimu aliyekuwa anagombea ubunge Jimbo la Kinondoni.

Mnyika alisema watakuwa mstari wa mbele, hawataogopa mabomu na wakipiga kura wasiondoke vituoni.

Mdee alihamasisha apigiwe kura Mwalimu, akisema ahitaji kusimulia yanayomkumba kila mmoja kutokana na utawala wa awamu ya tano.

Sumaye alisema CCM hawana huruma na wananchi, wakipata kura wanawaacha, wananunua wabunge kwa kodi za wananchi.

Dk. Mashinji alisema Usalama wa Taifa badala ya kufanya intelijensia kuangalia uchumi unavyokua, wanaiangalia Chadema inafanya nini.

Mbowe alisikika akisema Magufuli mwepesi kama karatasi, ataongoza mapambano ya kutafuta haki na kwamba watu wamepotea akiwemo Ben Saanane.

Mwalimu aliomba wananchi wampigie kura apate ushindi na kuwa mbunge wa Kinondoni.

Video ilionyesha Mbowe akiwaeleza wananchi kwamba muda huo ulikuwa saa kumi na mbili, mawakala wao hawajapata barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, akasema wanakwenda kufuata barua hizo na aliwauliza wananchi anayehitaji kuambatana nao.

Wananchi walionekana wanaondoka katika viwanja vya Buibui, lakini viongozi wa Chadema wakiwemo wabunge hawakuonekana katika video hiyo hadi inamalizika.

Upande wa utetezi unawakilishwa na Peter Kibatala, Profesa Abdallah Safari na Fred Kihwelo.

KESI YA MSINGI

Katika kesi ya msingi, Mbowe na wenzake wanadaiwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai, ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Inadaiwa Februari 16, mwaka huu, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam Bulaya alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huu, Barabara ya Kawawa, eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja, washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa jeshi la polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni wakati wa mkutano wa hadhara, mshtakiwa Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki.

Alidaiwa kutamka maneno “Kesho patachimbika, upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii… wizi unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano… watu wanapotea… watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome… ” yaliyoelekea kuleta chuki kati ya Serikali na Watanzania.

KIBATALA vs KOPLO CHARLES

Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, Koplo Charles alidai hafahamu kama kulichukia Jeshi la Polisi ni kosa la jinai na hafahamu kuhusu mtu anayeitwa Ben Saanane, mwandishi wa habari Anzory Gwanda na Mdude Nyagali.

Alidai anamfahamu Tundu Lissu na alishambuliwa kwa risasi, lakini hafahamu alishambuliwa akiwa eneo gani na pia hafahamu kama kitendo cha kushambuliwa Lissu kililichafua jeshi hilo.

Kibatala alihoji kama shahidi anafahamu maana ya kuchinja inavyotumika katika uchaguzi, na alijibu hafahamu ila alisikia Mdee akisema watamchinja Magufuli.

Shahidi alidai hajui kama kadi ya kupigia kura inaitwa kichinjio katika uchaguzi na hafahamu kama mawakala wa Chadema hadi saa 12 Februari 16, mwaka jana walikuwa hawajapewa barua na msimamizi wa uchaguzi Kinondoni.

Kesi itaendelea leo kwa upande wa utetezi kumuhoji shahidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles