27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo TPDC wafutiwa kesi

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemwachia huru Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Petroli la Tanzania (TPDC), James Mataragio na vigogo wenzake wanne baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuomba kufanya hivyo.

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kesi ilikuja kwa kusikilizwa, lakini DPP amewasilisha hati akionyesha hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Wankyo aliomba mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwaachia huru washtakiwa na kwamba hati ya kuliondoa shauri hilo ilitolewa tangu Julai 10, mwaka huu.

Upande wa utetezi haukuwa na pingamizi kwa maombi hayo na mahakama ilikubali hoja za Jamhuri na kuwaachia huru washtakiwa.

Washtakiwa wote walikuwa wanadaiwa kutenda makosa kati ya Aprili 8, 2015 na Juni 3, 2016.

Inadaiwa wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC, kwa nafasi zao wakati wakitimiza majukumu yao, kwa makusudi walitumia madaraka vibaya.

Kwamba walibadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa manunuzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha airborne gravity gradiometer survey ndani ya Ziwa Tanganyika bila ya kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi ya shirika.

Inadaiwa kitendo hicho kinakiuka kifungu cha 49(2) cha sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyo halali ya Dola za Marekani 3,238,986.50.

Washtakiwa walioachiwa huru ni Mataragio, George Seni, aliyekuwa Kaimu Meneja wa Uvumbuzi, Welington Hudson, aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Utawala, Kelvin Komba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu na Edwin Riwa, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mipango.

Kesi hiyo ilifikia hatua ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini baada ya Rais Dk. John Magufuli kuamuru Mataragio kurejeshwa kazini, Jamhuri imefikia uamuzi wa kuiondoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles