Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wamekubaliana mambo saba yakiwamo suala la kuondolewa kwa vikwazo kwa Zimbabwe, kufuatilia hali ya usalama nchini Congo na ombi la Burundi kujiunga na jumuiya hiyo.
Mengine ni kuwekeza kwenye miundombinu itakayowezesha kukua kwa uchumi katika ukanda wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, kuwa na chombo cha kukabiliana na majnga na suala la upatikanaji wa mapato.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano huo wa SADC wa siku mbili uliomalizika leo Jumapili Agosti 18, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hotuba ya kuhitimisha mkutano huo, Rais Dk. John Magufuli amesema wakuu wa nchi wamekubaliana kuendelea kufuatilia hali ya usalama nchini Congo lakini pia wameiagiza sekretarieti kuharakisha chombo cha kukabiliana na majanga kitakachosaidia nchi wanachama kukabiliana na majanga kama vile njaa, mafuriko, vimbunga, magonjwa ya mlipuko na mengineyo.
Amesema katika mkutano huo pia, wakuu wa nchi walipitia hali ya uchumi katika ukanda wao ambapo uchumi wa nchi hizo ulishindwa kukua kama ulivyotarajiwa kwa asilimia saba na kushuka hadi asilimia 3.1, hivyo wamekubaliana kuwekeza kwenye miundombinu kwa kuwa ni mojawapo ya kikwazo cha kukua kwa uchumi kwenye bara la Afrika ikiwamo nchi za SADC.
“Kwa pamoja tumekubaliana kuondoa viwazo vya kibiashara, ukiritimba katika maeneo ya mipakani na rushwa. “Aidha tumekubaliana kuboresha mazingira ya ukuaji uchumi na fedha katika nchi zetu.
“Masuala mengine tuliyojadili ni upatikanaji wa mapato, suala la ombi la Burundi kujiunga na SADC pamoja na suala la vikwazo kwa Zimbabwe,” amesema Rais Dk. Magufuli.
Kuhusu suala la Burundi kujiunga na jumuiya hiyo, amesema bado haijakamilisha vigezo katika baadhi ya maeneo ambapo Sekretarieti ya jumuiya hiyo imeagiwa kuwaelekeza na kisha kutuma tena maombi hayo na kuhusu Zimbabwe amesema wamekubaliana kufuatilia jumuiya za kimataifa ili iwaondolee vikwazo.
Pamoja na mambo mengine, amesema mkutano huo pia umepitisha mpango wa kuongeza mapato kwa SADC ambapo nchi wanachama zitakuwa na hiyari ya kuchagua njia bora ya kuchangia.