27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Makinda arusha kombora UWT

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

SPIKA mstaafu wa Bunge, Anne Makinda amesema Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) wa sasa ni tofauti na ule ulioasisiwa wakati wa kupigania uhuru kwani umetawaliwa na ubinafsi.

Makinda aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, kwenye ziara ya Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake  ya nchini Kenya, ambayo ilimtembelea mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria nyumbani kwake, Msasani Dar es Salaam kwa nia ya  kumuenzi Nyerere na kumkabidhi tuzo na zawadi mbalimbali.

Miongoni mwa wanawake hao wa Kenya waliomtembelea Mama Maria ni pamoja na  mwanaharakati maarufu nchini humo ambaye pia ni mwandishi wa vitabu, Muthoni Likimani (94), Phoebe Asiyo ambaye ni muasisi wa umoja huo.

Wengine ni Zipporah Kittony na Winfred Mwendwa ambaye alipata kuwa Waziri mwanamke wa kwanza katika serikali ya Kenya na aliyeshiriki pamoja na Mama Getrude Mongella wa Tanzania katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Beijing nchini China wa kupigania haki za wanawake.

Katika ziara yao hiyo iliyoratibiwa na mwanasiasa na mpigania haki za wanawake maarufu nchini, Mongella, kiongozi huyo mstaafu wa Bunge,  Makinda alihoji matendo ya sasa ya UWT kama yangezaa 50 kwa 50 inayoshuhudiwa sasa.

Zaidi aliinyooshea kidole kwa kushindwa kuwaenzi na kuwathamini viongozi walioasisi umoja huo wa wanawake ambao kwa sasa ni wazee.

“Siku moja nilienda UWT walinialika, nikawauliza je wanawakumbuka waliopigania wanawake kwa sababu UWT ya wakati ule haikuwa ya chama bali UWT asili ambayo ilituleta sisi sote tulioko leo hapa” alisema Makinda ambaye mbali na kuambatana na Mongella pia alikuwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, mwanasiasa mkongwe Kate Kamba na wengine.

Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda

Huku akiwataja kwa majina baadhi ya wanawake walioshiriki kuipigania UWT miaka ya nyuma kama Tekla Gumbo na mwingine aliyeko Kimara ambaye alisema jina lake ameliandika mahali, alisema alipouliza juu ya taarifa kama hizo alijibiwa hazipo jambo ambalo ni kosa.

 “Sasa hawa waliopigania mambo ya wanawake wakati ule ni tofauti na leo tunavyopigania mambo ya wanawake kwa sababu sasa tumejaza ubinafsi.

“Kama tungeendelea na mtindo waliofanya hawa, leo 50 kwa 50 mngekuwa hamzungumzi ingekuwa wazi 50 ungekumbatia peke yako, haiwezekani!

“Sasa ni sawa kweli hawa wamama kutoka Kenya na umri wao kupanda ndege? Naomba Tanzania na Kenya tuondoe ubinafsi maana siku hizi kila mtu anafikiria yeye atakuwa nani kama ni nafasi hizi zinapita.

“Naomba tusibakie na utaalamu tulionao tukaenda nao kaburini hautakuwa na manufaa lakini tukiweza kuacha kwa watu wengine utaendelea kuzaa, ni vyema tutengeneze ‘document’ ili wajukuu waje wasome huko mbeleni,” alisema Makinda.

Makinda ambaye alipata kuwa mbunge kwa muda mrefu kabla ya kuwa spika, alisema namna nchi zinavyoweza kushirikiana ni watu na sio marais wala mawaziri ambao wao kazi yao mara nyingi ni kuandika mikataba ambayo siku moja itatupwa.

“Lakini mkataba wa mama hawa kwa umri wao wamepanda ndege, hauwezi kukatika kwa sababu hata wakiondoka vijana mmeona kuwa kuna wamama kutoka Kenya walikuja huu ni undugu ambao ni wa ndani wa damu kabisa hauhitaji mkataba.

“Na huu ndio undugu unaweza hata kuchukua akili zao na mawazo yao, hakuna kitu chenye thamani kubwa kama watu kutembeleana na kuonana na kuongea na kushauriana bila mikataba ya kwenye makaratasi,”alisema Makinda.

Mwenyekiti wa Umoja wa Maendeleo ya Wanawake Kenya, Rahabu Muiu alisema wanawake wa nchini humo wameungana bila kuweka itikadi za aina yoyote.

“Kenya tulikuwa na muungano maarufu ‘handshake’ baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga walikutana na kuamua kushirikiana hivyo na sisi wanawake tumeungana na kuachana mambo ya uvyama.

“Kupitia Pan African Women Organization (PAWO), tungetaka mara nyingine sauti ya mwanamke kupitia kwako Mama Maria Nyerere usikike na ufike katika mkutano wa viongozi wa Muungano wa Afrika (AU), ili masuala muhimu ya wanawake katika bara hili yashughulikiwe na kutekelezwa na viongozi wetu,”alisema Muiu.

Kwa upande wake, mpigania uhuru na mwanaharakati wa Kenya Muthoni aliwataka wanawake kuacha siasa za chuki kwa sababu tayari walishamuondoa mkoloni hivyo hakuna haja ya kushambuliana wenyewe kwa wenyewe.

“Kina mama fujo ikitokea msijiingize huko, mkatae fujo na kutosikilizana kwa sababu nchi ni ya kila mtu. Ni lazima mhakikishe ninyi ni waunganishaji hata mtu akikusema usipambane naye. Msimame kidete na msitukane mtu hata mmoja,”alisema.

Kwa upande wake, Mama Maria Nyerere aliwashukuru wanawake hao kwa kumtembelea huku akisema wajisikie wako nyumbani

Awali baada ya Makinda kuzungumza,  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alikiri kuwa hawakufanya vizuri katika kuwaenzi wanawake wazee ambao ni waasisi wa umoja huo.

Kwa upande wake, Waziri Ummy alisema kupitia ugeni huo kutoka Kenya na hasa uamuzi wao kwa kufika kwa ajili ya kumuenzi Mama Maria Nyerere, imewapa changamoto wizara yake hivyo watafanya utaratibu ili waandae kila mwaka mara moja waweze kuwaenzi wanawake.

“Ni kweli kama wizara yetu hatukufanya vizuri katika kuwaenzi wazee, nakuahidi (Maria Nyerere) tutatafuta kila mwaka kukaa na wazee waliopigania nchi hii. Ujio wa wageni wako umetupa changamoto sisi wizara, naahidi hilo tutalifanyia kazi,”alisema Ummy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles