Na Frederick Katulanda, Mwanza
ALIYEKUWA mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa ameonekana kutishwa na nguvu kubwa inayotumiwa na polisi kudhibiti wafuasi wa chama hicho.
Lowassa amesema anashangazwa na jeshi hilo kumwaga askari wengi wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, marehemu Alphonce Mawazo.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Mwanza jana.
Alisema kitendo cha polisi kudhibiti wafuasi wa chama hicho kwenye msiba huo ni mwendelezo wa hatua za Serikali kuwabana watu na makada waliokuwa wakiunga mkono wagombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)wakati wa uchaguzi mkuu.
Polisi wanapaswa kutambua ubabe wanaoufanya hausaidii nchi hii ambayo inaweza kuendesha mambo yake bila ya kuwa na polisi, alisema.
“Nimetishwa na wingi wa polisi waliomwaga hapa wakiwa na magari ya deraya.
“Nashauri iwapo wanadhani wanao askari wengi wasio na kazi wawapunguze kuliko kukusanya askari wengi kwa ajili ya kuzuia haki ya msingi ya familia na wanachama kuaga mwili na kufanya ibada,”alisema.
Alisema matumizi ya magari ya maji ya kuwasha kwenye msiba huo yanaonyesha Serikali iliyanunua kwa gharama kubwa lakini hayana kazi ya kufanya.
“Serikali imenunua magari haya kwa gharama kubwa, sasa ni wazi yanaonekana hayana kazi ya kufanya, wanayaleta kwenye misiba.
“Uchaguzi umemalizika waliyofanya wamefanya, tumewashauri watu wetu kutulia, wanaanza kufuatiliwa.
“Kwa mfano kule Mpwapwa kuna kada wetu mmoja amefuatwa wamempandishia kodi kubwa amelazimika kufunga shule yake… tunawaomba viongozi msiingize nchi hii kwenye machafuko,” alisema.
MBOWE
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wamejadiliana kwa kina kama chama, kwamba hawajaridhishwa na sababu zilizotolewa na polisi Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa Wilaya wa Geita za kuwataka kumzika marehemu Mawazo bila kumuaga wala kumfanyia ibada.
Akionekana kukerwa na hatua hiyo, Mbowe alihoji mbona wasanii wanapofariki dunia huagwa kwenye viwanja vya wazi.
“Mawazo hakuwa kibaka, muhuni; alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Katibu Mwenezi wa Kanda ya Ziwa yenye makao makuu yake Mwanza, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama pia alikuwa mgombea ubunge, wanatuzuiaje kumuaga kwenye uwanja wa wazi ama ofisi za chama?” alihoji Mbowe.
Alisema viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao hufariki dunia, wamekuwa wakiagwa kwenye viwanja vya wazi na vya michezo.
Alitoa mfano wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda,marehemu Dk. Abdalah Kigoda ambaye aliagwa Dar es Salaam na kuzikwa mkoani Tanga.
“Leo (jana),polisi wamejipa mamlaka ya kutuzuia kufanya ibada na kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi wetu na kufunga ofisi zetu za kanda kwa siku tatu wakilinda usiku na mchana…sasa baada ya mashauriano tumeamua kulipeleka jambo hili mahakamani,” alifafanua.
Alisema chama kwa kushirikiana na familia, wameamua kufungua kesi Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza kuiomba kulitolea uamuzi suala hilo na kwamba kwa muda wote viongozi wa Chadema wataendelea kuishi Mwanza.
Tamko la familia
Mchungaji Charles Lugiko ambaye ni baba wa marehemu, alisema amesikitishwa na kitendo cha polisi kuwafukuza waombolezaji ambao walikusanyika nyumbani kwake Nyegezi Sweya kwa ajili ya kushiriki msiba huo.
Alisema familia imehuzunishwa na hatua hiyo na kwa kauli moja wameamua kushirikiana na Chadema kutafuta haki mahakamani.
“Tulileta mwili wa kijana wangu Mwanza kwa kuwa awali tulitaka kuzika huku, baada ya kujadiliana na mama yake tulikubalina tukamzike kijijini Chikobe alikozaliwa. Cha ajabu nimezuiliwa kufanya msiba nimeambiwa nisifanye ibada eti kuna ugonjwa wa kipindupindu,” alisema.
Alisema anapinga uamuzi wa polisi na ndiyo maana wameamua kulifikisha suala hilo mahakamani.
SHUHUDA
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Saidi Issa Mohamed alisema kwa siku mbili alikuwa mkoani Geita ambako alipata bahati ya kuonana na familia ya marehemu Mawazo na kufuatilia ukweli wa tukio hilo.
Alisema polisi wamekuwa wakipewa taarifa za watuhumiwa wa mauaji hayo lakini wameshindwa kuwakamata, hivyo kulazimisha vijana wa Chadema kuwakamata na kuwapeleka kituo cha polisi.
Alisema wakati Mawazo akishambuliwa walikuwapo watu wawili ambao ni ndugu; walishuhudia kila kitu kilichokuwa kikifanyika.
“Hawa mashuhuda wanasema wauaji walikuwa na gari ambalo namba zake za usajili wanazo. Walimteka Mawazo na kumuingiza katika gari lao, kisha kumweka barabarani ambako walitaka kumkanyaga kwa gari…lakini hushuda huyo polisi hawataki kumsikiliza.
“Kwa kutambua hili, chama kimeamua kumhifadhi kwa sababu anawajua hata majina wahusika wa mauaji haya,” alisema.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alionya kuwa nguvu kubwa inayotumiwa na vyombo vya dola inaweza kuliingiza taifa kwenye machafuko.
“Haki inapotoweka usitegemee kuendelea amani…nchi hii iliridhia kuwapo mfumo wa vyama vingi lazima wajue vinakuwa kwa kasi na wasitarajie kuvimaliza kwa kutumia dola, hii ni hatari,” alisema.