31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wamtisha Lowassa

Pg 2Na Frederick Katulanda, Mwanza

ALIYEKUWA mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa ameonekana kutishwa na nguvu kubwa inayotumiwa na   polisi kudhibiti wafuasi wa chama hicho.

Lowassa  amesema anashangazwa na jeshi hilo kumwaga askari wengi wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, marehemu Alphonce Mawazo.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Mwanza jana.

Alisema kitendo cha polisi  kudhibiti wafuasi wa chama hicho kwenye msiba huo ni mwendelezo wa hatua  za Serikali   kuwabana watu na makada waliokuwa wakiunga mkono wagombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)wakati wa uchaguzi mkuu.

Polisi wanapaswa kutambua  ubabe wanaoufanya hausaidii nchi hii ambayo  inaweza kuendesha mambo yake bila ya kuwa na polisi, alisema.

“Nimetishwa na wingi wa polisi waliomwaga hapa wakiwa na magari ya deraya.

“Nashauri iwapo  wanadhani wanao askari wengi wasio na kazi wawapunguze kuliko kukusanya askari wengi kwa ajili ya kuzuia haki ya msingi ya familia na wanachama kuaga mwili na kufanya ibada,”alisema.

Alisema matumizi ya magari ya maji ya kuwasha kwenye msiba huo yanaonyesha Serikali iliyanunua kwa gharama kubwa lakini hayana kazi ya kufanya.

“Serikali imenunua magari haya kwa gharama kubwa, sasa ni wazi yanaonekana hayana kazi ya kufanya, wanayaleta kwenye misiba.

“Uchaguzi umemalizika waliyofanya wamefanya, tumewashauri watu wetu kutulia, wanaanza kufuatiliwa.

“Kwa mfano kule Mpwapwa kuna  kada wetu mmoja amefuatwa wamempandishia kodi kubwa amelazimika  kufunga shule yake… tunawaomba viongozi msiingize nchi hii kwenye machafuko,” alisema.

MBOWE

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wamejadiliana kwa kina kama chama, kwamba hawajaridhishwa na sababu zilizotolewa na polisi  Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa Wilaya wa Geita za kuwataka kumzika marehemu Mawazo bila kumuaga wala kumfanyia ibada.

Akionekana kukerwa na hatua hiyo, Mbowe alihoji mbona wasanii wanapofariki dunia huagwa kwenye viwanja vya wazi.

“Mawazo hakuwa kibaka, muhuni; alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Katibu Mwenezi  wa Kanda ya Ziwa yenye makao makuu yake Mwanza, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama pia alikuwa mgombea ubunge, wanatuzuiaje kumuaga kwenye uwanja wa wazi ama ofisi za chama?” alihoji Mbowe.

Alisema viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao hufariki dunia, wamekuwa  wakiagwa kwenye viwanja vya wazi na vya michezo.

Alitoa mfano wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda,marehemu Dk. Abdalah Kigoda ambaye aliagwa Dar es Salaam na   kuzikwa mkoani Tanga.

“Leo (jana),polisi wamejipa mamlaka ya kutuzuia kufanya ibada na kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi wetu na kufunga ofisi zetu za kanda kwa   siku tatu wakilinda usiku na mchana…sasa baada ya mashauriano tumeamua kulipeleka jambo hili mahakamani,” alifafanua.

Alisema chama kwa kushirikiana na familia, wameamua kufungua kesi Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza  kuiomba   kulitolea uamuzi suala hilo na kwamba kwa muda wote viongozi wa Chadema wataendelea kuishi Mwanza.

 

Tamko la familia

Mchungaji Charles Lugiko ambaye ni baba wa marehemu, alisema amesikitishwa na kitendo cha polisi kuwafukuza waombolezaji ambao walikusanyika nyumbani kwake Nyegezi Sweya kwa ajili ya kushiriki msiba huo.

Alisema  familia imehuzunishwa na hatua hiyo na kwa  kauli moja wameamua kushirikiana na Chadema kutafuta haki mahakamani.

“Tulileta mwili wa kijana wangu Mwanza kwa kuwa awali tulitaka kuzika huku, baada ya kujadiliana na mama yake tulikubalina tukamzike kijijini Chikobe alikozaliwa.  Cha ajabu nimezuiliwa kufanya msiba nimeambiwa nisifanye ibada eti kuna ugonjwa wa kipindupindu,” alisema.

Alisema anapinga uamuzi wa polisi na ndiyo maana wameamua kulifikisha suala hilo mahakamani.

 

SHUHUDA

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Saidi Issa Mohamed alisema  kwa   siku mbili alikuwa mkoani Geita ambako alipata bahati ya kuonana na familia ya marehemu Mawazo na kufuatilia ukweli wa tukio hilo.

Alisema polisi wamekuwa wakipewa taarifa za watuhumiwa wa mauaji hayo lakini wameshindwa kuwakamata, hivyo kulazimisha vijana wa Chadema kuwakamata na kuwapeleka kituo cha polisi.

Alisema wakati   Mawazo akishambuliwa walikuwapo  watu wawili ambao ni ndugu; walishuhudia kila kitu kilichokuwa kikifanyika.

“Hawa mashuhuda wanasema wauaji walikuwa na gari ambalo namba zake za usajili wanazo.  Walimteka   Mawazo na kumuingiza katika gari lao, kisha kumweka barabarani ambako walitaka kumkanyaga kwa gari…lakini hushuda huyo polisi hawataki kumsikiliza.

“Kwa kutambua hili, chama kimeamua kumhifadhi kwa sababu anawajua hata majina wahusika wa mauaji haya,” alisema.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alionya kuwa nguvu kubwa inayotumiwa na vyombo vya dola inaweza kuliingiza taifa kwenye machafuko.

“Haki inapotoweka usitegemee kuendelea  amani…nchi hii iliridhia kuwapo mfumo wa vyama vingi lazima wajue vinakuwa kwa kasi na wasitarajie kuvimaliza kwa kutumia dola, hii ni hatari,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles