WASHINGTON, MAREKANI
MAOFISA wa ujasusi nchini Marekani wamesema Hamza ambaye ni mtoto wa kiume wa mwasisi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda, Osama bin Laden, ameuawa katika shambulio la anga.
Hata hivyo maofisa hao hawajaeleza mahala au tarehe ya kifo cha Hamza.
Makao makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Pentagon nayo haijaeleza chochote.
Taarifa za kifo cha Hamza zimeripotiwa kwa upana na vyombo vya habari vya Marekani kikiwemo kituo cha NBC News, gazeti la New York Times na kituo cha televisheni cha CNN, vyote vikinukuu chanzo cha taarifa hizo pasipo kutaja jina kuwa ni maofisa wa usalama wa Marekani.
Februari mwaka huu Serikali ya Marekani iliahidi kutoa dola milioni moja kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kutambua alipo.
Hamza bin Laden, anayedhaniwa kuwa na umri wa miaka 30, alikuwa ametoa ujumbe mbalimbali wa sauti na video akitoa wito wa kufanya mashambulio dhidi ya Marekani na nchi nyingine.
Inaelezwa kuwa Hamza kabla ya mauti yake aliwahi kutoa wito kwa wapiganaji wa Jihad kulipiza kisasi dhidi ya wale waliohusika na mauaji ya baba yake aliyeuliwa na kikosi maalumu cha Marekani nchini Pakistan Mei 2011.
Machi, mwaka jana, katika taarifa yake ya mwisho kwa umma alitoa wito wa kulipa kisasi dhidi ya watu wa rasi ya Saudi Arabia kwa kuwa nchi hiyo ilimyang’anya uraia.
Inaaminika kuwa Hamza alizaliwa Jeddah, Saudi Arabia kabla ya kutumia miaka mingi akiwa na mama yake nchini Iran.
Aliaminika kuwa katika kifungo cha nyumbani nchini Iran lakini ripoti nyingine zilisema kuwa huenda alikuwa akiishi katika mataifa ya Afghanistan, Pakistan na Syria.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema nyaraka zilizokamatwa katika uvamizi wa mwaka 2011 katika nyumba ya baba yake ya Abbottabad, Pakistan, zilionyesha kuwa Hamza alikuwa anaandaliwa kuchukua utawala wa al-Qaeda.
Vikosi vya Marekani pia viliripotiwa kubaini video ya harusi yake akimuoa binti wa ofisa mwingine wa ngazi ya juu wa al-Qaeda ambayo ilidhaniwa kufanyika nchini Iran.
Baba mkwe wake alikuwa ni Abdullah Ahmed Abdullah au Abu Muhammad al-Masri, ambaye anatafutwa kwa madai ya kuhusika katika mashambulio ya ugaidi ya mwaka 1998 dhidi ya balozi za Tanzania na Kenya.
Al-Qaeda ni kundi lililotekeleza mashambulio mabaya ya ugaidi ya Septemba 11, 2001 dhidi ya Marekani, lakini hadhi yake kwa sasa imeshuka katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita baada ya kuibuka kwa umaarufu wa kundi la Islamic State.
Inaelezwa kuwa Hamza alikuwa ni mtoto pekee aliyekuwepo wakati baba yake aliposaidia kupanga njama za mashambulio ya Septemba 11.
Kwa mujibu wa wakuu wa kundi hilo lenye itikadi kali, alikuwa pamoja naye wakati wa mashambulio hayo.
Katika miaka ya hivi karibuni, Hamza alituma ujumbe mtandaoni akitoa wito kwa mashambulio dhidi ya Marekani na washirika wake.
Baba yake Osama bin Laden alifahamika nchini Afghanistan katika miaka ya 1980, kama mwarabu aliyejitolea kujiunga na kikosi cha Afghanstan kilichoungwa mkono na mujahideen kilichopigana kuvifukuza vikosi vilivyoteka eneo la Usovieti
Alianzisha shirika la kusaidia wahudumu wa kujitolea ambalo lilikuja kutambuliwa kama al-Qaeda, au “ngome”.
Aliondoka Afghanistan mwaka 1989, na kurejea tena mwaka 1996 kuongoza kambi za mafunzo ya kijeshi ya maelfu ya waislamu kutoka mataifa ya kigeni.
Al-Qaeda ilitangaza “vita vitakatifu ” dhidi ya Wamarekani,wayahudi na washirika wao.