24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

China yashtushwa kontena la msaada kufika tupu Kenya

Nairobi, Kenya

CHINA imeeleza kushtushwa na taarifa iliyopokea kutoka kwa Bunge la Kenya, kuwa kontena lililokuwa na vifaa ilivyovitoa kwa nchi hiyo kama msaada na kuwasili Jumanne iliyopita, lilifunguliwa na maofisa wa bunge hilo na kukutwa likiwa tupu.

China imesema tukio hilo ni la kwanza kuwahi kutokea, na kwamba kwa miaka mingi imekuwa ikitoa misaada ya kirafiki kwa Kenya, ikiwemo vifaa tiba, vifaa vya ofisi, msaada wa chakula na kadhalika, na vyote vimekuwa vikiwasilishwa vikiwa salama kabisa.

Vifaa vilivyokuwa katika kontena hilo ambavyo vimeorodheshwa ni pamoja na kompyuta mpakato, na projekta ambazo zilikuwa msaada kutoka Bunge la Taifa la China na mzigo huo ulipaswa kufikishwa Kenya kupitia ubalozi wa China nchini humo.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limezungumza na msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kenya, Charles Owino kuhusu taarifa za kuwasili kwa kontena kutoka kwenye viwanja vya Bunge likiwa tupu na kueleza kuwa hana taarifa kabisa kuhusu jambo hilo isipokuwa kupitia mitandao.

”Kwa kawaida huwa tunapata briefing kutoka kwa mkuu wa polisi na sijui kama ni mambo ya mitandao ya kijamii ama ni kweli kwa sababu sijapata taarifa kwa mkuu wa upelelezi hivyo pengine niulizie halafu baadae tuweze kuzungumza,” alisema.

Alisema pia hana habari kama kontena hilo liliwasili likiwa tupu.

Taarifa zinaeleza kuwa tayari uchunguzi unafanywa na Idara ya makosa ya jinai nchini Kenya kubaini mazingira yaliyojitokeza  kontena hilo kutoka China kuwasili Kenya likiwa tupu.

Tukio hili limewagusa raia wengi wa Kenya, huku baadhi wakisema ni jambo lililoaibisha nchi hiyo.

Televisheni ya Citizen ya Kenya iliripoti kuwa katika taarifa iliyowasilishwa juzi, Karani wa Bunge la Kenya, Michael Sialai alithibitisha kuwa kontena lililowekwa nembo ya ‘mizigo ya kidiplomasia’ liliwasili Jumanne, Julai 30, 2019 kama ilivyotarajiwa, lakini baada ya kufunguliwa, hakukuwa na kitu ndani yake. 

Kwa mujibu wa karani wa Bunge la Kenya, ubalozi wa China jijini Nairobi iliingia mkataba na kampuni ya usafirishaji ya M/S Bollore Africa Transport & Logistics Ltd kusafirisha kontena hilo.

”Kweli kontena liliwasili katika viwanja vya Bunge tarehe 30 mwezi Julai, 2019, ambapo niliwateua maofisa kadhaa kutoka kwenye Bunge waweze kuthibitisha mzigo kwa ulinganifu na kile kilichoelezwa kuwasilishwa na ubalozi wa China,” ilieleza taarifa ya Sialai.

”Baada ya kufungua kontena, ilithibitishwa kuwa lilikuwa tupu. Wakala na maofisa wetu kwa pamoja walinifikishia suala hilo na kuamua kuwa maafisa wa DCI wapatiwe taarifa hiyo, suala ambalo lilifanyika ipasavyo”.

Baada ya uthibitisho kuwa kontena lililowasilishwa na kampuni ya M/S Bollore Africa Transport & Logistics Ltd lilikuwa tupu, maafisa wa DCI waliripotiwa kutoa taarifa kwa ubalozi wa China wakati uchunguzi ukiendelea.

Kutolewa kwa msaada wa vifaa vya elektroniki kwa ajili ya Bunge kuliwekwa wazi wakati wa ziara ya makamu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge la watu wa China na ujumbe wa maafisa wa China Aprili 13 mwaka huu. 

Hakuna uthibitisho kuhusu mahali au lini vifaa hivyo vya kielektroniki ambavyo thamani yake haijafahamika vilitolewa na kutoweka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles