27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kudhibitiwa

Aveline Kitomary -Dar es salaam

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  imesema inaandaa mpango mkakati mpya ili kuhakikisha wanadhibiti na kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yanayoathiri zaidi familia masikini.

Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni pamoja na trankoma, kichocho, mabusha, usubi, minyoo ya tumbo na mengineyo.

Akizungumza katika mkutano wa  mwaka wa mapitio wa shughuli za kitaifa za kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa wa Wizara ya Afya,  Dk. Elias Kwesi, alisema kupitia mkutano huo wa siku mbili watatengeneza  mkakati mpya.

“Tunafanya ‘review’ (mapitio) ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele ili kutengeneza mpango mkakati mpya, hapa tunakutana na wadau mbalimbali wa afya katika mkutano huu wa siku mbili, tutahakikisha tunatoka na mkakati mpya,” alisema Dk. Kwesi.

Alisema watajadili changamoto za utekelezaji  wa mradi uliopita na kuweka mpango wa kutatua changamoto hizo.

“Katika kuhakikisha kupata mkakati mpya, kwanza tutahakikisha kujua na kujadili changamoto za utekelezaji wa mradi uliopita  na kuweka mpango wa kutatua changamoto hizo,” alisema Dk. Kwesi.

Alisema Wizara ya Afya imefanikiwa kupunguza magonjwa hayo ndani ya miaka 10 na kufikia asilimia 80 na kwamba Serikali hutumia dola za Marekani milioni 11 kwa mwaka.

“Kama Serikali, tumefanikiwa  kupunguza idadi ya wilaya  zinazokabiliwa na magonjwa hayo. Ilikuwa wilaya 71, sasa hivi tumebakiwa na wilaya 24. Upande wa upasuaji mabusha zoezi linaendelea mikoa ya Lindi, Tanga, Dar es Salaam, sasa wapo Nachingwea.

“Pia tumekutana na wadau kama WHO kuangalia ni jinsi gani tutamudu gharama kwani mradi mzima unagharimu dola milioni 20. Hata hivyo tumefanikiwa kupunguza, ndani ya miaka 10 tumefikia asilimia 80, tunaendelea kupambana kumaliza hiyo 20 iliyobaki,” alisema Dk. Kwesi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Taifa wa Magonjwa  yaliyokuwa hayapewi kipaumbele,  Dk. Upendo Mwingira, alisema changamoto kubwa ipo katika magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo hasa kwa watoto  wa umri wa kwenda shule.

“Bado tuna changamoto, lakini kwa kiwango kikubwa tumeweza kufanikiwa kudhibiti magonjwa hayo, tuna changamoto katika magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo tunatakiwa tuendelee kuwakinga wananchi,  hasa watoto wa umri wa kwenda shule,” alisema Dk. Mwingira.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dk. Leon Ard.subi , alisema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuelewa namna maambukizi yanavyotokea na kujikinga na magonjwa hayo.

“Kuna magonjwa kama kuumwa na nyoka yamesahaulika, nyoka wana sumu kali japo hatuna takwimu kwa sababu watu wanapoumwa hawafiki hospitali, hivyo tunaendelea kutoa elimu namna ya kujikinga na magonjwa hayo, hasa trakoma ukinawa uso vizuri huwezi kupata,” alisema Dk.Ard.subi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles