Hadija Omary -Lindi
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amekagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.
Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa na yuko jimboni kwake kwa mapumziko mafupi, alikagua ujenzi huo jana.
Jengo la ofisi hizo linalojengwa na Suma JKT, linahitaji Sh bilioni 3.77 hadi kukamilika.
Akiwa kwenye eneo la ofisi hizo, Majaliwa alielezwa kwamba halmashauri hiyo imepokea Sh milioni 500 kutoka Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2018/19 kwa ujenzi wa ofisi hiyo mpya.
Ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja, ulianza Juni mosi 2019 na unatarajiwa kukamilika Julai, mwakani ambapo litakuwa na ofisi 33 za chini, ofisi 26 za ghorofa ya kwanza na kumbi mbili za mikutano.
Kazi ambazo zimeshafanyika hadi sasa ni usafishaji wa eneo la ujenzi, upimaji wa sampuli ya udongo, uingizaji maji, uchimbaji kisima kikubwa cha kuhifadhia maji na uvutaji umeme.
Kazi zinazoendelea kwa sasa ni ufyatuaji wa tofali ambapo hadi sasa jumla ya matofali 10,000 yamekwishafyatuliwa ambayo ni sawa na asilimia 50 ya mahitaji. Pia ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi eneo la ujenzi unaendelea.
Majaliwa pia alikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na kukiri kwamba ameridhishwa na kazi iliyokwishafanyika hadi sasa.
Akiwa hospitalini hapo, alielezwa na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk. Mahela Njile kwamba hadi kukamilika kwake, hospitali hiyo itakuwa na majengo 22 yanayokisiwa kugharimu Sh bilioni 7.5 kulingana na maksio ya Ofisi ya Rais Tamisemi.
Dk. Njile alisema katika awamu ya kwanza Serikali imetoa Sh bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la uzazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, X-ray, utoaji dawa, kufulia nguo na utawala.
“Serikali imeelekeza ujenzi huu ufanyike kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’ ambapo halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa kujenga majengo yaliyoelekezwa, wakisimamiwa na wataalamu wa halmashauri na kamati mbalimbali,” alisema Dk. Njile.
Akizungumza na wakazi waliojitokeza kumsikiliza hospitalini hapo, Majaliwa aliwapongeza viongozi wa halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi na kwa kuamua kutumia force account ambayo alisema inapunguza gharama za manunuzi.