27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tuhuma za rushwa kwa DC Sabaya zakutanisha wawekezaji, uongozi Mkoa wa Kilimanjaro

Upendo Mosha -Moshi

IKIWA zimepita siku chache baada Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya kutuhumiwa kudai rushwa ya Sh milioni 10 kwa mfanyabiashara wa utalii wa Kampuni ya Asante Tours, Cathberty Swai, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro imekutana na wawekezaji na wafanyabiashara wa wilaya hiyo kusikiliza kero zao.

Pia tayari Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro imekutana na kufanya mazungunzo na mkuu huyo wa wilaya kutokana na tuhuma zinazomkabili.

Hatua hizo zinakuja wakati ikielezwa kuwa Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ilishaanza uchunguzi juu ya tuhuma hizo.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwhira, alisema hatua moja ya kuzungumza na Sabaya imeshafanyika na hatua ya pili iliyofuata ni kamati hiyo kukutana na wafanyabiashara hao kusikiliza madai yao ya tuhuma za rushwa na kunyanyaswa na mkuu huyo wa wilaya.

“Tumekuwa na muda mzuri wa kukutana na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Wilaya ya Hai, lengo letu si kutafuta mchawi, bali ni kufanya suluhu ya changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa utendaji kazi wa Serikali,” alisema Mgwhira.

Alisema baada ya hatua hiyo ya kuwasikiliza wafanyabiashara na wawekezaji, hatua itakayofuata ni kukutana pande zote mbili ili mwafaka uweze kufikiwa na kuondoa malalamiko ambayo kwa sasa yameendelea kushamiri.

“Sisi tulichofanya ni kuwasikiza tu na baada ya hapa tutawakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara ambao wana madai na kero dhidi ya Mkuu wa Wilaya ili kumaliza migogoro na tofauti zao,” alisema.

Hata hivyo kilichojadiliwa kwenye kikao hicho kilichodumu kwa zaidi ya saa tano kimebaki kuwa ni siri.

Aidha Mgwhira aliwataka watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kufuata kanuni za utumishi wa umma jambo ambalo litaondoa madai ya rushwa.

Mmoja wa wawekezaji kutoka katika wilaya hiyo, Jenestine Natai, alisema hatua ya Serikali kuwaita wawekezaji na wafanyabiashara ni jambo la msingi na kwamba litazidi kuimarisha mshikamano.

 “Tunashukuru mkuu wa mkoa kutukutanisha na kutusikiliza kero ambazo tunaamini zikifanyiwa kazi zitafungua ukurasa mpya katika utendaji wetu kwani baadhi ya kero zinatusababisha sisi kushindwa kufanya kazi kwa amani,” alisema. 

Pamoja na madai ya kumlalamikia mkuu huyo wa wilaya, wafanyabiashara na wawekezaji hao pia wamekuwa wakilalamikia utendaji kazi dhahifu miongoni mwa taasisi za Serikali, ikiwemo Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Juma lililopita mfanyabiashara wa utalii wa Kampuni ya Asante Tours, Cathberty Swai, alimtuhumu Sabaya kumpa vitisho na kudai fedha kwa nguvu ikiwa ni pamoja na kuwakamata wafanyakazi wake na kuwaweka mahabusu.

Mfanyabiashara huyo alisema hayo katika kikao cha wafanyabiashara na TR), kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Swai alidai mkuu huyo wa wilaya amekuwa ni kikwazo kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Alidai licha ya kulipa kodi serikalini ambayo kwa mwaka huwa analipa Sh milioni 148, lakini amekuwa akipokea vitisho na manyanyaso kutoka kwa mkuu huyo wa wilaya na kumlazimisha kumpa fedha.

Swai alidai mara kwa mara Sabaya amekuwa akivamia katika hoteli yake ya kitalii ya Weruweru River Lodge usiku kwa madai kuwa anakusanya kodi.

Alidai kuwa Sabaya akiwakuta wafanyakazi na wakashindwa kumpa majibu, huwachukua na kuwaweka mahabusu bila sababu za msingi.

“Nimesema haya nikiwa sijui hatma yangu itakuwaje, lakini mpaka sasa nimeshampa Sh milioni 10 na alikuja na kufanya fujo ambapo nilikuwa na mteja wangu mwenye wafuasi zaidi ya elfu 30,000, alimsumbua sana,” alidai.

Hata hivyo, Sabaya alikana tuhuma hizo.

“Tuhuma hizo zimetengenezwa na hazina ukweli wowote wala sijawahi kumwoba rushwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles