26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa apokea msaada wa Sh mil 25

Mwandishi Wetu -Ruangwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka benki ya NMB vyenye thamani ya Sh milioni 25.

Vifaa hivyo ni fremu 46 za madirisha ya aluminium na vioo vyake, milango 18, mabati 56, misumari na mbao, kompyuta 10, madaftari 4,050 vyote vikiwa na thamani ya Sh  milioni 25.

Akipokea msaada huo  jana Zhanati ya Nandagala, wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Majaliwa aliwashukuru viongozi wa benki hiyo kwa kuamua kuchangia.

Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Nandagala, Majaliwa ambaye ni Mbunge wa Ruangwa, alisema mchango uliotolewa unamaanisha kazi ya kukamilisha jengo la wodi ya wagonjwa na vyumba vya madaktari, lazima ifanyike haraka.

“Tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NMB kwa msaada huu mkubwa. Hii maana yake lazima tuharakishe kukamilisha jengo hili ili tuanze kutoa huduma kwa wananchi wa Nandagala na vijiji vya jirani.

“Tulianza na ujenzi wa zahanati, kisha tukajenga jengo la upasuaji lenye wodi mbili, moja ya wanaume na nyingine ya wanawake ambazo kila moja ina uwezo wa kulaza wagonjwa 20 kwa wakati mmoja,” alisema.

Jengo  jipya ambalo ujenzi wake ukikamilika litakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 60.

Aliwataka wakazi hao wafikirie uwezekano wa kujenga wodi nyingine na pamoja na jiko ili wagonjwa watakaokuwa wanalazwa hapo, wapate mahali pa kupikiwa chakula.

Mapema, akitoa taarifa ya msaada huo, Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikali katika Benki ya NMB, Vicky Bishubo, alisema kipaumbele cha benki hiyo kila mara ni kutatua changamoto za afya na elimu kwani sekta hizo ni nguzo kuu ya maendeleo kwa taifa lolote.

“Vitu hivi tunavyokabidhi leo ni moja ya ushiriki wetu katika maendeleo ya jamii na sisi kama benki inayoongoza Tanzania, tunahakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika kutokana na faida tunayoipata,” alisema.

Alisema mwaka huu, benki imetenga zaidi ya Sh  bilioni moja kuchangia maendeleo ya jamii, ikiwamo kusaidia sekta ya afya na elimu.

“Mpaka ninavyoongea leo, tayari tumetoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 600 kwa mwaka huu wa 2019 tu,” alisema.

Akielezea kuhusu programu ya Jifunze, Jipange na Wajibika (Wajibu), Bishubo alisema hadi sasa wameshawafikia vijana wasiopungua 42,000 katika shule za msingi na sekondari kwa kuwapa elimu ya fedha na kujifunza kuweka akiba katika umri mdogo kupitia programu hiyo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nandagala, Andrew Chikongwe, aliishukuru benki hiyo kwa kuwasaidia vifaa hivyo ambavyo alisema vimefika kwa wakati mwafaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles