CLARA MATIMO- MWANZA
WIZARA ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imewaagiza maofisa elimu mikoa na wakurugenzi wa halmashauri, kuhakikisha walimu waliopandishwa madaraja, wanalipwa stahiki zao kuanzia Agosti.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Tixon Nzunda, alipotembelea shule za Msingi Bukumbi na Kigongo zilizopo wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza.
Shule hizo mbili zilikuwa zikitekeleza mradi wa fursa kwa watoto tangu mwaka 2014 hadi 2018 kwa ufadhili wa Shirika la Children in Crossfire (CIC) linalojihusisha na malezi na makuzi ya awali ya watoto kwa kushirikiana na Shirika la Uchumi wa Nyumbani (Tahea).
Agizo hilo alilitoa kutokana na malalamiko ya baadhi ya walimu wa shule hizo waliodai wamepandishwa madaraja lakini miezi mitano imepita na hawajaanza kulipwa mishahara mipya.
“Simamieni nyie wenyewe (maofisa elimu) kuhakikisha walimu wanabadilishiwa mishahara yao maana wapo baadhi ya maofisa utumishi wavivu, wakurugenzi hakikisheni kila mwezi mnaingia kwenye mfumo kuangalia kwasababu wanaweza kutengeneza mazingira ya rushwa ili kutoa stahiki hizo.
“Kama wewe ni kiongozi lakini kazi yako ni kukandamiza wenzako wasifanikiwe you are not a leader (siyo kiongozi), tunataka viongozi ambao wanawezesha wanaowaongoza kufanikiwa, nawaagiza nyie ambao mnawaongoza hawa walimu kushughulikia nyongeza yao ya mishahara,” alisema.
Nzunda alisema kitendo cha walimu hao kutoongezewa mishahara ni kutenegeneza malimbikizo ambayo hawatayapata kwa wakati, kuwaumiza kisaikolojia na kuipa Serikali mzigo wa madeni.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Msingi Ofisi ya Raisi-TAMISEMI, George Jidamva, aliwataka maofisa elimu kujenga ukaribu na walimu ili kubaini changamoto zinazowakabili ili kuongeza ufaulu kwa asilimia 100.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa CIC, Craig Ferla, alisema mradi wa fursa kwa watoto ambao wameutekeleza katika wilaya ya Misungwi, Ilemela na Nyamagana za Mkoani Mwanza na Kilimanjaro, ulilenga kuwafikia watoto 25,000 lakini umevuka lengo na kuwafikia 37,000.