LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Walter Nnko, amesema mtu yeyote atakayetangaza vita dhidi ya Rais Dk. John Magufuli ajue ametangaza vita na wananchi kutokana na mambo mazuri ambayo ameyafanya kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ya uongozi wake.
Dk. Nnko ambaye mwaka 2015 alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza nia ya kutaka kugombea ubunge katika jimbo la Kawe na kupigwa chini katika kura za maoni baada ya kushika nafasi ya tano ametoa kauli hiyo Dar es Salaam leo Alhamisi Julai 25, katika mkutano na waandishi wa habari.
Amesema ana imani kwamba Watanzania wengi wanafuatilia kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano na Rais Dk. Magufuli mwenyewe ambazo zinaonesha kuwa ana upendo mkubwa na nchi yake.
“Kwa kweli Rais wetu mpendwa ameonesha upendo mkubwa kwa nchi yetu, ni dhahiri mapenzi yake kwa Taifa letu ni makubwa kupitiliza. Miaka mitatu imekuwa ni yenye mafanikio makubwa sijawahi kuona kwa serikali zote zilizopita.
“Nadiriki kusema kwa Serikali zote zilizopita kwa kipindi cha miaka mitatu hazijawahi kufanya maendeleo makubwa kama haya yanavyoonekana sasa hivi na wala sitajisikia vibaya kusema hivyo kwa sababu kila Mtanzania anaona yanayofanywa” amesema Dk. Nnko.
Amesema kwa miaka kadhaa Tanzania ilikuwa na shirika la ndege ambalo lilibaki jina kutokana na kutokuwa na ndege lakini sasa ndege za mashirika mengine zinaporuka na za Tanzania zinaruka na zinapotua hutua zote.
Amesema kutokana na mafanikio hayo wananchi wanapaswa kutambua kuwa vita yoyote inayopigwa na Rais ni vita ya watanzania wote na si vita yake peke yake.
Amesema hata sasa Serikali imeweza kuheshimika kutokana na kupungua kwa rushwa, ufisadi na vitendo vingine vinavyoweza kushusha heshima ya Serikali.
Amesema kwa wale wachache ambao pengine wanatafuta kulipwa fadhila watambue sasa si muda wake badala yake wasaidie katika kuliletea taifa maendeleo.