FLORENCE SANAWA, MTWARA
Benki ya NMB imewahamasisha wafanyabiashara mkoani mtwara kuongeza mitaji kwa kukopa, ili kuweza kupiga hatua kiuchumi ambapo imepanga kuongeza fursa za uwekezaji kwa kupeleka baadhi ya wafanyabiashara nchini China.
Akizungumza na wafanyabiashara Mkoani humo, Mkuu wa Kitengo cha Biashara NMB Donatus Richard alisema wafanyabiashara wa kitanzania wapelekwe nchini China ili kujifunza fursa mbalimbali za kibiashara zikiwemo za uwekezaji wa viwanda kuendana na kasi ya Tanzania ya viwanda.
Alisema kuwa wafanyabiashara hao mbali na fursa wataenda kujifunza Katika Nyanja mbalimbali ili kujua namna gani wanaweza kufanya biashara kimataifa hatua ambayo itawanyanyua kiuchumi.
“Tumekuwa tukitoa mafunzo mbalimbali kwa wajasiriamali ikiwa ni pamoja na kutunza rekodi, masoko namna ya kujisajili kibiashara ndio maana tunaamini kuwa wakienda nchini China wakajifunza zaidi wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu na katika safari hiyo tunatarajia kupeleka wafanyabiashara 10” alisema.
“Wapo wafanyabiashara walioanza kukopa shilingi milioni mbili lakini leo hii ni mabilionea ukiwaongezea ujuzi na maarifa kwa kuwapa mafunzo mbalimbali na kuwakutanisha na wafanyabiashara mbalimbali wanaweza kuwa chanzo kizuri cha kuinua uchumi wa taifa letu” alisema Richard