33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Raia watatu wauawa kwa risasi, askari kwa kwa mawe

DAMIAN MASYENENE-MWANZA

WATU wanne, akiwamo Ofisa Mfawidhi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Ukerewe, Ibrahim Jalali, wameuawa katika vurugu zilizozuka juzi kati ya wananchi na askari, Kisiwa cha Siza, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa 9 hadi 10 jioni katika kisiwa hicho ambacho sehemu kubwa ya wananchi wake ni wavuvi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Cornel Magembe, alisema askari huyo aliuawa kwa kushambuliwa kwa mawe na wananchi.

Alisema hadi sasa watu watatu wanashikiliwa wakihusishwa na tukio hilo.

Magembe alisema Serikali haitoruhusu kuona watumishi wake wanazuiwa kutekeleza majukumu yao na kwamba yeyote anayehusika atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Alisema askari mmoja aliyejeruhiwa amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure kwa matibabu zaidi, huku mwananchi mmoja aliyejeruhiwa kwa risasi akiendelea kutibiwa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, Bomani.

“Ni kweli jana kulitokea tukio la mauaji katika Kisiwa cha Siza kinachokaliwa na wavuvi kwa asilimia kubwa, ilitokea ugomvi baina ya wananchi ambao ni wavuvi na kikosi cha doria majira ya saa 10 jioni,” alisema Magembe.

Alisema kikosi hicho kilichokuwa na askari saba, kilifika eneo hilo na kuanza kufanya shughuli iliyowapeleka, lakini wananchi wakawazuia na kuanza kumshambulia kwa mawe mkuu wa kikosi, Jalali hadi walipomuua.

 “Baada ya hapo wakaanza tena kuwashambulia askari. Katika juhudi za kujiokoa, askari mmoja alifyatua risasi, kwa bahati mbaya ikawapata wananchi wanne, ambao watatu walifariki papo hapo na mmoja kujeruhiwa,” alisema Magembe.

Alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ilifika eneo la tukio na kukuta watu wameshatawanyika.

“Tuliwahi katika eneo lile, lakini tukakuta wananchi wametawanyika, jana (juzi) tumekamata watu watatu wanaoshukiwa kuhusika na jambo hili na wanaendelea kuhojiwa, pia tunaendelea na msako na tuna matumaini tutawakamata wote.

“Tunaendelea na uchunguzi kubaini undani na chanzo cha tukio hili, kama Serikali tunalaani vikali jambo hili, haikubaliki kuwazuia watumishi wa Serikali kufanya ama kutimiza wajibu wao na kuanza kuwashambulia,” alisema.

Awali juzi jioni, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema mamlaka zinaendelea na uchunguzi wa jambo hilo kubaini chanzo kwani taarifa za awali zilizopo zinaeleza kuwa vurugu ndizo zilizosababisha mauaji hayo.

“Mchana wa leo (juzi) tulipata taarifa kutoka Wilaya ya Ukerewe, Kisiwa cha Siza karibu na kisiwa kikubwa cha Ghana, kulikuwa na doria ya kupambana na uvuvi haramu, baada ya kufika pale kulitokea mzozo kati ya timu nzima ya kikosi cha kudhibiti uvuvi haramu na wananchi.

“Kwa sababu yoyote ile iwayo, mwananchi ama mtu yeyote hatakiwi kujeruhuiwa ama kuumizwa bila sababu ya msingi, kama Serikali tunaendelea kufanya uchunguzi, yeyote anayehusika atakabiliwa kisheria.

“Vyombo vinaendelea na uchunguzi kubaini sababu zaidi, hakuna atakayeonewa, nitoe pole kwa familia za marehemu, na kama Serikali tunaendelea kufanya taratibu na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya tayari iko kule, imeagizwa ibaki huko kujiridhisha mpaka usalama na utulivu utakaporejea, pia Kamati ya Mkoa ilitarajiwa kwenda kule Jumanne,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles