33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

AAR wachangia damu, watoa huduma za afya bure

MANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya Bima ya AAR na Taasisi ya Damu Salama zimeshirikiana tukio la kuchangia damu eneo la Ukonga, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Taasisi hizo ambazo ni wadau muhimu wa sekta ya afya nchini, pia zilitoa huduma ya kupima afya za wakazi wa eneo hilo bure na kutoa huduma nyingine za kitabibu ikiwa ni pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu afya.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukamilika tukio hilo, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni ya Bima ya AAR, Hamida Rashid alisema kuwa hiyo ni sehemu ya utamaduni wa taasisi hizo kujali afya ya jamii na kushiriki kwa vitendo kuboresha na kulinda maisha yao.

“Tunaendeleza utamaduni wetu wa kujali ustawi wa jamii kwa sababu uwepo wetu unatokana na jamii inayotuzunguka. Hivyo, kama wadau muhimu wa sekta ya afya, tumeamua kushiriki kwa vitendo kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya jamii yenye uhitaji.

 “Tunafahamu kuna uhitaji mkubwa wa damu salama nchini na ni jukumu letu kama kampuni ya bima kushirikiana na wadau wenzetu, Damu Salama kushiriki kwa vitendo katika upatikanaji wa damu,” alisema Hamida.

Alisema kuwa taasisi hizo zimetoa huduma nyingine za afya ikiwa ni pamoja na ushauri wa kitabibu kwa wakazi wa Mombasa-Ukonga kwani wanaamini kuwa jamii inapaswa kupata elimu ya kutosha ya jinsi ya kujikinga na magonjwa na kuimarisha afya zao ili kupunguza idadi ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa yatokanayo na kutozingatia au kutofahamu masuala ya msingi ya kuimarisha afya zao.

Mtaalamu mwelekezi wa uchangiaji damu kutoka Damu Salama, Mariam Juma, alisema pamoja na kuchangia damu, taasisi hizo zimetumia fursa hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu namna bora ya kuimarisha afya zao, faida ya kuchangia damu na kuhuisha usalama wa damu ili kuongeza upatikanaji wa damu salama.

Mkazi wa Mombasa Ukonga, Lister Gilbert, ambaye ni mmoja kati ya walioshiriki kuchangia damu, alizipongeza taasisi hizo kwa jinsi zilivyoendesha zoezi hilo kwa kutoa elimu iliyomwongezea sababu zaidi za kuchangia damu.

Mwishoni mwa Juni, mwaka huu, Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) ilieleza kuwa kwa mwaka jana Tanzania ilikuwa na upungufu wa damu kwa asilimia 42, ikieleza kuwa kupitia uchangiaji damu nchini, kiasi cha chupa 307,835 kilipatikana ambacho ni sawa na asilimia 58 ya mahitaji.

Kwa mujibu wa NBTS, ili kukidhi mahitaji ya kila mwaka, taasisi hiyo inapaswa kukusanya chupa 526,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles