23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mufti awataka mahujaji kutekeleza ibada kwa vitendo

CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

MUFTI wa Tanzania, Sheikh Aboubakary Zuberi, amewataka mahujaji nchini kutumia safari za hijja kutekeleza ibada na kutojihusisha na vitendo visivyofaa ikiwamo kuzungumzia mambo ya kisiasa.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa mahujaji yaliyoandaliwa na Idara ya Hijja Bakwata Makao Makuu, wanaotarajiwa kuanza safari kwenda Makka na Madina, Agosti 4.

Mufti alisema kila hujaji kabla ya safari ni lazima atie nia kitu gani anakifuata katika ibada hiyo ili kujenga uhusiano mkubwa na Mwenyezi Mungu.

Alisema kinyume na matakwa hayo, Mungu hawezi kupokea ibada zao endapo wataenda kujishughulisha na kujiingiza katika mambo machafu.

“Maana ya hijja ni kuomba rehema ya msamaha kwa matendo tuliyoyafanya, haitapendeza endapo mtafika huko na kuanza kuzungumzia siasa, hili halitampendeza Mwenyezi Mungu,” alisema Mufti Zuberi.

Alisema jambo la msingi ni kuhakikisha wanakuwa watulivu na kuacha maovu waliyokuwa wakiyafanya hapa nchini ambayo mengi yanawatenga na Mungu.

“Kikubwa mkiwa huko nawaombeni mjikitize zaidi katika ibada kwani hiyo ndiyo nguzo ya tano ya Uislamu pamoja na kuombea nchi amani na Rais Dk. John Magufuli ili hata mkirejea muwe na amani pia,” alisema.

Alisema hadi sasa tayari wamesajili mahujaji 110 ingawa wanataraji kusajili mahujaji 2,000.

“Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), tayari limesajili mahujaji 110  ambao wengi wao wapo mikoani, lengo ni kusafirisha mahujaji 120 na usajili bado unaendelea,” alisema.

Mkurugenzi wa Hijja Bakwata, Alhaj Haidari Kambwili,  alisema mahujaji hao watarejea nchini Agosti 25, na wamejipanga kuhakikisha hawapati usumbufu wa makazi.

Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Jongo,  alisisitiza hijja hiyo itumike kiibada zaidi na kuweka kando mazungumzo ya kisiasa.

Alisema gharama za hijja kwa mwaka huu kwa wanaoanza ni dola za Marekani 4,300 na watakaorudia dola 4,500.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles